Matendo
28 Na tulipokuwa tumefaulu kufika kwenye usalama, ndipo tukapata habari kwamba hicho kisiwa kiliitwa Malta. 2 Na hao watu wenye kusema lugha ya kigeni wakatuonyesha fadhili ya kibinadamu isiyo ya kawaida, kwa maana waliwasha moto na kutupokea sisi sote kwa njia ya kusaidia kwa sababu ya mvua iliyokuwa ikinyesha na kwa sababu ya baridi. 3 Lakini Paulo alipokusanya tita fulani la vijiti na kuliweka juu ya moto, nyoka-kipiri akatoka kwa sababu ya joto na kujifungilia mwenyewe kwenye mkono wake. 4 Hao watu wenye kusema lugha ya kigeni walipoona mara hiyo huyo kiumbe mwenye sumu akining’inia kwenye mkono wake, wakaanza kuambiana: “Hakika mtu huyu ni muuaji-kimakusudi, na ingawa alifaulu kufika kwenye usalama kutoka baharini, haki yenye kudai kisasi haikumruhusu afulize kuishi.” 5 Hata hivyo, yeye akakung’uta huyo kiumbe mwenye sumu ndani ya moto na hakupatwa na dhara. 6 Lakini wao walikuwa wakitarajia atavimba kwa sababu ya mwasho au kwa ghafula aanguke akiwa mfu. Baada ya wao kungojea kwa muda mrefu na kuona kwamba hakuna jambo lolote lenye kuumiza lililotukia kwake, wakabadili maoni yao na kuanza kusema yeye ni mungu.
7 Sasa katika ujirani wa mahali hapo mtu aliye mkubwa wa hicho kisiwa, aitwaye jina Publio, alikuwa na mashamba; naye akatupokea kwa ukaribishaji-wageni na kutupokea kwa hisani siku tatu. 8 Lakini ikatukia kwamba baba ya Publio alikuwa amelala akitaabishwa na homa na ugonjwa wa kuhara damu, na Paulo akaingia alimo na kusali, akamwekea mikono yake akamponya. 9 Baada ya hili kutukia, watu wale wengine kisiwani waliokuwa na magonjwa wakaanza pia kumjia na kuponywa. 10 Nao pia wakatuheshimu kwa zawadi nyingi na, tulipokuwa tukisafiri kwa mashua, wakatupakilia vitu kwa ajili ya mahitaji yetu.
11 Miezi mitatu baadaye tukasafiri kutoka Aleksandria kwa mashua iliyokuwa imekaa wakati wa majira ya baridi katika hicho kisiwa na yenye sanamu ya gubeti ya “Wana wa Zeusi.” 12 Nasi tukiegesha kuingia bandarini katika Sirakusi tukakaa siku tatu, 13 mahali ambapo kutoka hapo tulienda tukizunguka na kuwasili Regiamu. Na siku moja baadaye upepo wa kusini ukazuka nasi tukafaulu kuingia Puteoli siku ya pili. 14 Hapa tukakuta akina ndugu na tukasihiwa sana tukae pamoja nao siku saba; na kwa njia hii tukaja kuelekea Roma. 15 Na kutoka huko akina ndugu, waliposikia habari juu yetu, wakaja kukutana nasi hadi Mahali pa Sokoni Apio na Mikahawa Mitatu na, alipowaona mara hiyo, Paulo akamshukuru Mungu na kujipa moyo. 16 Mwishowe, tulipoingia katika Roma, Paulo akaruhusiwa kukaa akiwa peke yake pamoja na askari-jeshi mwenye kumlinda.
17 Hata hivyo, siku tatu baadaye akawaita pamoja wale waliokuwa ndio watu walio wakubwa wa Wayahudi. Walipokuwa wamekusanyika, akaanza kuwaambia: “Wanaume, akina ndugu, ijapokuwa sikuwa nimefanya jambo lolote kinyume cha watu au desturi za baba zetu wa zamani, nilikabidhiwa nikiwa mfungwa kutoka Yerusalemu kuingizwa mikononi mwa Waroma. 18 Na hawa, baada ya kufanya uchunguzi, walikuwa wenye kutaka kunifungua, kwa kuwa hakukuwa na sababu yoyote ya kifo kwangu. 19 Lakini Wayahudi walipofuliza kusema vibaya juu ya hilo, nilishurutika kukata rufani kwa Kaisari, lakini si kama kwamba nilikuwa na jambo lolote la kushtakia taifa langu. 20 Kwa kweli kwa sababu hii nilisihi sana niwaone na kusema nanyi, kwa maana kwa sababu ya tumaini la Israeli nina mnyororo huu ukiwa wanizunguka.” 21 Wakamwambia: “Wala sisi hatujapokea barua zinazokuhusu wewe kutoka Yudea, wala hakuna yeyote wa akina ndugu ambaye amewasili aliyeripoti au kusema jambo lolote ovu juu yako. 22 Lakini sisi twafikiri yafaa kusikia kutoka kwako fikira zako ni nini, kwa maana kweli kwa habari ya farakano hili yajulikana kwetu kwamba kila mahali huwa lasemwa vibaya.”
23 Basi wakapanga siku fulani ya kuwa pamoja naye, nao wakamjia wakiwa idadi kubwa zaidi mahali pake pa kukaa. Naye akawaeleza hilo jambo kwa kutoa ushahidi kamili kuhusiana na ufalme wa Mungu na kwa kutumia ushawishi kwao kuhusu Yesu kutoka katika sheria ya Musa na pia Manabii, tangu asubuhi hadi jioni. 24 Na wengine wakaanza kuamini mambo yaliyosemwa; wengine wakawa hawaamini. 25 Kwa hiyo, kwa sababu walikosa kukubaliana, wakaanza kuondoka, huku Paulo akifanya elezo moja hili:
“Roho takatifu kwa kufaa ilisema kupitia Isaya nabii kwa baba zenu wa zamani, 26 ikisema, ‘Nenda kwa watu hawa na kusema: “Kwa kusikia, mtasikia lakini msielewe kamwe; na, kutazama, mtatazama, lakini msione kwa vyovyote. 27 Kwa maana moyo wa watu hawa umekuwa usioitikia, na kwa masikio yao wamesikia bila itikio, nao wamefunga macho yao; ili wasione kamwe kwa macho yao na kusikia kwa masikio yao na kuelewa kwa moyo wao na kurudi, nami niwaponye.”’ 28 Kwa hiyo acheni ijulikane kwenu kwamba hii, njia ambayo kwayo Mungu huokoa, imepelekwa nje kwa mataifa; wao wataisikiliza hakika.” 29 ——
30 Kwa hiyo akakaa miaka miwili mizima katika nyumba yake mwenyewe ya kukodiwa, naye akawa akiwapokea kwa fadhili wote wale walioingia ndani kwake, 31 akiwahubiri ufalme wa Mungu na kufundisha mambo yahusuyo Bwana Yesu Kristo kwa uhuru wa usemi ulio mkubwa zaidi sana, bila kizuizi.