Matendo
4 Sasa hao wawili walipokuwa wakisema na watu, makuhani wakuu na kapteni wa hekalu na Masadukayo wakawajia, 2 wakiwa wameudhika kwa sababu wao walikuwa wakiwafundisha watu na walikuwa wakiutangaza waziwazi ufufuo kutoka kwa wafu katika kisa cha Yesu; 3 nao wakawawekea mikono yao ili kuwashika na kuwaweka kifungoni hadi siku iliyofuata, kwa maana tayari ilikuwa jioni. 4 Hata hivyo, wengi kati ya wale waliokuwa wamesikiliza huo usemi wakaamini, na idadi ya wanaume ikawa karibu elfu tano.
5 Siku iliyofuata kukawa katika Yerusalemu kikusanyiko cha watawala wao na wanaume wazee na waandishi 6 (pia Anasi kuhani mkuu na Kayafa na Yohana na Aleksanda na wengi waliokuwa watu wa jamaa ya huyo kuhani mkuu), 7 nao wakawasimamisha katikati yao na kuanza kuulizia habari: “Ni kwa nguvu gani au ni katika jina la nani nyinyi mlifanya hilo?” 8 Ndipo Petro, akiwa amejazwa roho takatifu, akawaambia:
“Watawala wa watu na wanaume wazee, 9 ikiwa katika siku hii sisi tunachunguzwa, juu ya msingi wa kitendo chema kwa mtu mwenye kuugua, kuhusu ni nani ameponya mtu huyu, 10 acheni ijulikane kwenu nyote na kwa watu wote wa Israeli, kwamba katika jina la Yesu Kristo Mnazareti, ambaye nyinyi mlimtundika mtini lakini ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, kwa yeye mtu huyu asimama hapa akiwa timamu mbele yenu. 11 Hilo ni ‘jiwe lililotendwa na nyinyi wajenzi kama lisilo la maana ambalo limekuwa ndicho kichwa cha pembe.’ 12 Zaidi ya hilo, hakuna wokovu katika mwingine yeyote, kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu ambalo limepewa miongoni mwa watu ambalo kwalo lazima sisi tupate kuokolewa.”
13 Sasa walipoona usemi wa waziwazi wa Petro na Yohana, na kufahamu kwamba walikuwa watu wasio na elimu na wa kawaida tu, wakaanza kustaajabu. Nao wakaanza kutambua juu yao kwamba walikuwa na kawaida ya kuwa pamoja na Yesu; 14 nao walipokuwa wakitazama mtu aliyekuwa ameponywa akiwa amesimama pamoja nao, hawakuwa na la kusema kwa kukanusha. 15 Kwa hiyo wakawaamuru waende nje ya jumba la Sanhedrini, nao wakaanza kushauriana, 16 wakisema: “Tutafanya nini na watu hawa? Kwa sababu, kwa kweli, ishara mashuhuri imetukia kupitia wao, moja iliyo dhahiri kwa wakaaji wote wa Yerusalemu; nasi hatuwezi kuikana. 17 Hata hivyo, ili isipate kusambazwa zaidi kotekote miongoni mwa watu, acheni tuwaambie kwa matisho wasiseme tena kamwe juu ya msingi wa jina hili kwa mtu yeyote hata kidogo.”
18 Ndipo wakawaita na kuwaamuru, popote wasifanye tamko lolote wala kufundisha juu ya msingi wa jina la Yesu. 19 Lakini kwa kujibu Petro na Yohana wakawaambia: “Kama ni jambo la uadilifu mbele ya macho ya Mungu kuwasikiliza nyinyi badala ya Mungu, hukumuni nyinyi wenyewe. 20 Lakini kwa habari yetu, sisi hatuwezi kukoma kusema juu ya mambo ambayo tumeyaona na kuyasikia.” 21 Kwa hiyo, walipokuwa wamewatisha zaidi, wakawafungua, kwa kuwa hawakupata msingi wowote wa kuwaadhibu na kwa sababu ya watu, kwa sababu wote walikuwa wakimtukuza Mungu juu ya lililokuwa limetukia; 22 kwa maana mtu ambaye ishara hiyo ya kuponywa ilikuwa imetokea juu yake alikuwa na umri wa zaidi ya miaka arobaini.
23 Baada ya kufunguliwa wakaenda kwa watu wao wenyewe na kuripoti mambo yale ambayo makuhani wakuu na wanaume wazee walikuwa wamewaambia. 24 Waliposikia hilo wao kwa umoja wakamwinulia Mungu sauti zao na kusema:
“Bwana Mwenye Enzi Kuu, wewe Ndiwe uliyefanya mbingu na dunia na bahari na vitu vyote vilivyo ndani yazo, 25 na uliyesema kupitia roho takatifu kwa kinywa cha baba yetu wa zamani Daudi, mtumishi wako, ‘Kwa nini mataifa yakawa yenye fujofujo na vikundi vya watu vikatafakari juu ya mambo matupu? 26 Wafalme wa dunia walichukua msimamo wao nao watawala wakatungamana pamoja kama mtu mmoja dhidi ya Yehova na dhidi ya mtiwa-mafuta wake.’ 27 Ijapokuwa hivyo, Herode na pia Pontio Pilato pamoja na watu wa mataifa na pamoja na vikundi vya watu wa Israeli kwa kweli walikusanywa pamoja katika jiji hili dhidi ya mtumishi wako mtakatifu Yesu, ambaye ulimtia mafuta, 28 ili afanye mambo ambayo mkono wako na shauri viliagiza kimbele yatukie. 29 Na sasa, Yehova, yaangalie matisho yao, na kuwaruhusu watumwa wako kufuliza kusema neno lako kwa ujasiri wote, 30 huku ukinyoosha mkono wako ili kuponya na huku ishara nyingi na mambo ya ajabu yakitukia kupitia jina la mtumishi wako mtakatifu Yesu.”
31 Nao walipokuwa wameomba dua, hapo mahali walipokuwa wamekusanyika pamoja pakatikiswa; nao wote wakajazwa roho takatifu na wakawa wakisema neno la Mungu kwa ujasiri.
32 Zaidi ya hayo, umati wa waliokuwa wameamini ulikuwa na moyo na nafsi moja, na hakuna hata mmoja aliyekuwa akisema kwamba chochote cha vitu vilivyokuwa miliki yake kilikuwa chake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika. 33 Pia, wakiwa na nguvu kubwa mitume wakaendelea kutoa ushahidi kuhusu ufufuo wa Bwana Yesu; na fadhili isiyostahiliwa kwa kadiri kubwa ilikuwa juu yao wote. 34 Kwa kweli, hapakuwa hata mmoja mwenye uhitaji miongoni mwao; kwa maana wote wale waliokuwa wenye kumiliki mashamba au nyumba walikuwa wakiviuza na kuleta thamani za vitu vilivyouzwa 35 nao walikuwa wakiziweka kwenye miguu ya mitume. Nao ugawanyaji ulikuwa ukifanywa kwa kila mmoja, kama vile alivyokuwa na uhitaji. 36 Kwa hiyo Yosefu, aliyeitwa na mitume jina la ziada Barnaba, ambalo lamaanisha, litafsiriwapo, Mwana wa Faraja, Mlawi, mzaliwa wa Saiprasi, 37 akiwa anamiliki kipande cha shamba, akakiuza na kuzileta fedha na kuziweka kwenye miguu ya mitume.