Matendo
5 Hata hivyo, mwanamume fulani, Anania jina lake, pamoja na Safira mke wake, aliuza miliki 2 na kuzuia kisiri baadhi ya bei, mke wake pia akijua juu ya hilo, naye akaleta sehemu fulani tu na kuiweka kwenye miguu ya mitume. 3 Lakini Petro akasema: “Anania, kwa nini Shetani amekujasirisha wewe kufanya isivyo kweli kwa roho takatifu na kuzuia kisiri baadhi ya bei ya shamba? 4 Maadamu ilibaki na wewe je, haikubaki ikiwa yako, na baada ya kuuzwa je, haikuendelea kuwa katika udhibiti wako? Kwa nini ikawa kwamba ukakusudia kitendo kama hiki katika moyo wako? Umefanya isivyo kweli, si kwa wanadamu, bali kwa Mungu.” 5 Aliposikia maneno hayo Anania akaanguka chini akaisha. Na hofu kubwa ikaja juu ya wote wale wenye kusikia juu ya hilo. 6 Lakini wanaume vijana wakainuka, wakamfunga kwa vitambaa, na kumpeleka nje wakamzika.
7 Sasa baada ya muda wa karibu saa tatu mke wake akaingia, bila kujua lililokuwa limetukia. 8 Petro akamwambia: “Niambie, je, nyinyi wawili mliliuza shamba kwa kiasi hicho?” Akasema: “Ndiyo, kwa kiasi hicho.” 9 Kwa hiyo Petro akamwambia: “Kwa nini mlikubaliana kati yenu wawili kuijaribu roho ya Yehova? Tazama! Miguu ya wale waliozika mume wako ipo mlangoni, nao watakubeba kukupeleka nje.” 10 Mara hiyo, akaanguka chini kwenye miguu yake akaisha. Wale wanaume vijana walipoingia wakamkuta amekufa, nao wakambeba kumpeleka nje wakamzika kando ya mume wake. 11 Kwa sababu hiyo hofu kubwa ikaja juu ya kutaniko lote na juu ya wote wale wenye kusikia juu ya mambo haya.
12 Zaidi ya hayo, kupitia mikono ya mitume ishara nyingi na mambo ya ajabu yakaendelea kutukia miongoni mwa watu; nao wote walikuwa kwa umoja katika safu ya nguzo ya Solomoni. 13 Kweli, hakuna hata mmoja kati ya wale wengine aliyekuwa na moyo wa kujiunga mwenyewe nao; hata hivyo, watu walikuwa wakiwahimidi. 14 Zaidi ya hilo, waamini katika Bwana wakafuliza kuwa wakiongezwa, umati wa wanaume na pia wa wanawake; 15 hivi kwamba wakawaleta wagonjwa nje hata katika zile njia pana na kuwalaza huko juu ya vitanda vidogo na machela, ili, wakati Petro apitapo hapo, angalau kivuli chake kipate kuanguka juu ya mtu fulani kati yao. 16 Pia, umati kutoka kwenye majiji yenye kuzunguka Yerusalemu ukafuliza kuja pamoja, ukiwa umechukua wagonjwa na wale wenye kutaabika wakiwa na roho wasio safi, nao wote wakawa wakiponywa.
17 Lakini kuhani wa cheo cha juu na wote wale waliokuwa pamoja naye, lile farakano la Masadukayo lenye kuwako wakati huo, wakainuka na kuwa wenye kujawa na wivu, 18 nao wakawawekea mitume mikono ili kuwashika na kuwaweka mahali pa hadharani pa kifungo. 19 Lakini wakati wa usiku malaika wa Yehova akaifungua milango ya gereza, akawaleta nje na kusema: 20 “Shikeni njia yenu mwende, na, mkiisha kuchukua msimamo katika hekalu, fulizeni kusema na watu semi zote juu ya maisha haya.” 21 Baada ya kusikia hili, wakaingia hekaluni wakati wa mapambazuko na kuanza kufundisha.
Basi kuhani wa cheo cha juu na wale walio pamoja naye walipowasili, wakaita pamoja Sanhedrini na kusanyiko lote la wanaume wazee wa wana wa Israeli, nao wakatuma watu kwenye jela ili waletwe. 22 Lakini wakati wale maofisa walipofika huko hawakuwakuta katika gereza. Kwa hiyo wakarudi na kutoa ripoti, 23 wakisema: “Tuliikuta jela imefungwa kwa kufuli ikiwa na usalama wote na walindaji wakiwa wamesimama kwenye milango, lakini tulipofungua hatukukuta yeyote ndani.” 24 Basi, wakati kapteni wa hekalu na tena makuhani wakuu waliposikia maneno haya, wakafadhaishwa sana na mambo haya wasijue jambo hili lingekuwa nini. 25 Lakini mtu fulani akawasili na kuripoti kwao: “Tazameni! Wale watu mlioweka gerezani wako katika hekalu, wakiwa wamesimama na kuwafundisha watu.” 26 Ndipo kapteni akaenda zake pamoja na maofisa wake na kuendelea mbele kuwaleta, lakini bila jeuri, maana waliogopa kupigwa na watu kwa mawe.
27 Kwa hiyo wakawaleta na kuwasimamisha katika jumba la Sanhedrini. Na kuhani wa cheo cha juu akawauliza maswali 28 na kusema: “Tuliwaagiza hakika nyinyi msifulize kufundisha juu ya msingi wa jina hili, na bado, tazameni! mmejaza Yerusalemu fundisho lenu, nanyi mwaazimia kuileta damu ya mtu huyu juu yetu.” 29 Kwa kujibu Petro na wale mitume wengine wakasema: “Lazima sisi tumtii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu. 30 Mungu wa baba zetu wa zamani alimfufua Yesu, ambaye nyinyi mlimuua kikatili, mkimwangika juu ya mti. 31 Mungu alimkweza huyu kuwa Wakili Mkuu na Mwokozi kwenye mkono wake wa kuume, ili kuwapa Israeli toba na msamaha wa dhambi. 32 Nasi ni mashahidi wa mambo haya, na ndivyo roho takatifu, ambayo Mungu amewapa wale wanaomtii yeye akiwa mtawala.”
33 Waliposikia hili, wakahisi wamechomwa sana nao wakawa wakitaka kuwamaliza. 34 Lakini mtu fulani akainuka katika Sanhedrini, Farisayo aitwaye jina Gamalieli, mwalimu wa Sheria mwenye kustahiwa na watu wote, akatoa amri hao watu watolewe nje kwa muda kidogo. 35 Naye akawaambia: “Wanaume wa Israeli, jiangalieni nyinyi wenyewe kuhusu lile mkusudialo kufanya kwa habari ya watu hawa. 36 Kwa mfano, kabla ya siku hizi Theudasi aliinuka, akisema yeye mwenyewe alikuwa mtu wa maana, na idadi fulani ya wanaume, karibu mia nne, wakajiunga na chama chake. Lakini alimalizwa, na wote wale waliokuwa wakimtii wakatawanywa na kuja kuwa si kitu. 37 Baada yake Yudasi Mgalilaya aliinuka katika zile siku za usajili, naye akavuta watu wamfuate. Na bado mtu huyo aliangamia, na wote wale waliokuwa wakimtii wakatapanywa kotekote. 38 Na kwa hiyo, chini ya hali zilizopo, nawaambia nyinyi, Msijiingize katika mambo ya watu hawa, bali waacheni; (kwa sababu, ikiwa mpango huu au kazi hii ni kutoka kwa wanadamu, itapinduliwa; 39 lakini ikiwa ni kutoka kwa Mungu, hamtaweza kuwapindua;) ama sivyo, huenda mkaonwa kuwa wapiganaji dhidi ya Mungu kwa kweli.” 40 Ndipo wakamsikiliza, nao wakawaita mitume, wakawapiga viboko, na kuwaagiza wakome kusema juu ya msingi wa jina la Yesu, na kuwaacha waende zao.
41 Kwa hiyo, hawa wakashika njia yao kwenda kutoka mbele ya Sanhedrini, wakishangilia kwa sababu walikuwa wamehesabiwa wenye kustahili kuvunjiwa heshima kwa ajili ya jina lake. 42 Na kila siku katika hekalu na kutoka nyumba hadi nyumba wakaendelea bila kuacha kufundisha na kutangaza habari njema juu ya Kristo, Yesu.