Waroma
16 Napendekeza kwenu Fibi dada yetu, aliye mhudumu wa kutaniko lililo katika Kenkrea, 2 ili kwamba mpate kumkaribisha yeye katika Bwana katika njia ambayo yawastahili watakatifu, na kwamba nyinyi mpate kumsaidia katika jambo lolote ambalo katika hilo huenda akawahitaji, kwa maana yeye mwenyewe pia alithibitika kuwa mtetezi wa wengi, ndiyo, wa mimi mwenyewe.
3 Wapeni salamu zangu Priska na Akila wafanyakazi wenzangu katika Kristo Yesu, 4 ambao wamehatarisha shingo zao wenyewe kwa ajili ya nafsi yangu, ambao si mimi tu bali pia makutaniko yote ya mataifa yawashukuru; 5 na salimuni kutaniko lililo katika nyumba yao. Salimuni Epaineto mpendwa wangu, aliye matunda ya kwanza ya Asia kwa ajili ya Kristo. 6 Salimuni Maria, ambaye amefanya kazi nyingi za jasho kwa ajili yenu. 7 Salimuni Androniko na Yuniasi jamaa zangu na mateka wenzangu, ambao ni watu maarufu miongoni mwa mitume na ambao wamekuwa katika muungano na Kristo muda mrefu zaidi ya mimi.
8 Mpeni salamu zangu Ampliato mpendwa wangu katika Bwana. 9 Salimuni Urbano mfanyakazi mwenzetu katika Kristo, na Stakisi mpendwa wangu. 10 Salimuni Apelesi, aliye mkubaliwa katika Kristo. Salimuni wale wa kutoka nyumbani mwa Aristobulo. 11 Salimuni Herodioni aliye jamaa yangu. Salimuni wale wa kutoka nyumbani mwa Narkiso walio katika Bwana. 12 Salimuni Trifaina na Trifosa, wanawake wanaofanya kazi kwa bidii katika Bwana. Salimuni Persisi mpendwa wetu, kwa maana mwanamke huyo alifanya kazi nyingi za jasho katika Bwana. 13 Salimuni Rufo aliye mchaguliwa katika Bwana, na mama yake na yangu. 14 Salimuni Asinkrito, Flegoni, Hermesi, Patrobasi, Hermasi, na akina ndugu walio pamoja nao. 15 Salimuni Filologo na Yulia, Nereusi na dada yake, na Olimpasi, na watakatifu wote walio pamoja nao. 16 Salimianeni kwa busu takatifu. Makutaniko yote ya Kristo yawasalimu nyinyi.
17 Sasa nawahimiza nyinyi kwa bidii, akina ndugu, mfulize kuangalia wale wasababishao migawanyiko na sababu za kukwaza kinyume cha fundisho ambalo mmejifunza, na mwaepuke. 18 Kwa maana watu wa namna hiyo ni watumwa, si wa Bwana wetu Kristo, bali wa matumbo yao wenyewe; na kwa maongezi laini na usemi wa kusifu-sifu wao hushawishi mioyo ya wasio na hila. 19 Kwa maana utii wenu umekuja kujulikana na wote. Kwa hiyo nashangilia juu yenu. Lakini nataka nyinyi mwe wenye hekima kuhusu lililo jema, bali wasio na hatia kuhusu lililo ovu. 20 Kwa upande wake, Mungu apaye amani atamponda-ponda Shetani chini ya miguu yenu upesi. Fadhili isiyostahiliwa ya Bwana wetu Yesu iwe pamoja nanyi.
21 Timotheo mfanyakazi mwenzangu awasalimu nyinyi, na pia Lukio na Yasoni na Sosipateri jamaa zangu.
22 Mimi, Tertio, ambaye nimeufanya uandikaji wa barua hii, nawasalimu nyinyi katika Bwana.
23 Gayo, mkaribishaji wangu na wa kutaniko lote, awasalimu nyinyi. Erasto mtumishi-nyumba wa jiji awasalimu nyinyi, na ndivyo pia Kwarto ndugu yake. 24 ——
25 Sasa kwa yeye awezaye kuwafanya nyinyi imara kulingana na habari njema nitangazayo na kuhubiriwa kwa Yesu Kristo, kwa kupatana na ufunuo wa siri takatifu ambayo imewekwa kimya kwa nyakati zinazodumu muda mrefu 26 lakini sasa imefanywa dhahiri na kujulishwa kupitia maandiko ya kiunabii miongoni mwa mataifa yote kwa kupatana na amri ya Mungu adumuye milele ili kukuza utii kwa njia ya imani; 27 kwa Mungu, mwenye hekima peke yake, kuwe utukufu kupitia Yesu Kristo milele. Ameni.