Ufunuo
10 Nami nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amepambwa wingu, na upinde-mvua ulikuwa juu ya kichwa chake, na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake ilikuwa kama nguzo zenye moto, 2 na mkononi mwake alikuwa na hati-kunjo ndogo ikiwa imefunguliwa. Naye akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, lakini ule wake wa kushoto juu ya dunia, 3 naye akapaaza kilio kwa sauti kubwa kama vile wakati simba angurumapo. Na alipopaaza kilio, zile ngurumo saba zikatamka sauti zazo zenyewe.
4 Sasa wakati hizo ngurumo saba ziliposema, nilikuwa karibu kuandika; lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema: “Yatie muhuri mambo ambayo hizo ngurumo saba zilisema, na usiyaandike.” 5 Na malaika niliyemwona akiwa amesimama juu ya bahari na juu ya dunia akainua mkono wake wa kuume mbinguni, 6 na kwa Yeye aliye hai milele na milele, aliyeiumba mbingu na vitu vilivyo ndani yayo na dunia na vitu vilivyo ndani yayo na bahari na vitu vilivyo ndani yayo, akaapa: “Hakutakuwa kukawia tena kamwe; 7 lakini siku za kuvumisha kwa malaika wa saba, awapo karibu kupuliza tarumbeta yake, siri takatifu ya Mungu kulingana na habari njema aliyowatangazia watumwa wake mwenyewe hao manabii imeletwa kwenye tamati.”
8 Na sauti niliyosikia kutoka mbinguni inasema nami tena na kuniambia: “Nenda, uchukue hati-kunjo iliyofunguliwa iliyo mkononi mwa malaika ambaye amesimama juu ya bahari na juu ya dunia.” 9 Nami nikaenda zangu kwa huyo malaika na kumwambia anipe ile hati-kunjo ndogo. Naye akaniambia: “Ichukue uile kabisa, nayo itafanya tumbo lako kuwa chungu, lakini kinywani mwako itakuwa tamu kama asali.” 10 Nami nikachukua hiyo hati-kunjo ndogo kutoka mkononi mwa yule malaika na kuila kabisa, na kinywani mwangu ilikuwa tamu kama asali; lakini nilipokuwa nimeila kabisa, tumbo langu likafanywa kuwa chungu. 11 Nao waniambia: “Lazima utoe unabii tena kuhusiana na vikundi vya watu na mataifa na lugha na wafalme wengi.”