Ufunuo
11 Nami nikapewa tete kama fimbo aliposema: “Inuka upime patakatifu pa hekalu la Mungu na madhabahu na wale wanaoabudu ndani yalo. 2 Lakini kwa habari ya ua ulioko nje ya patakatifu pa hekalu, utupe nje kabisa na usiupime, kwa sababu mataifa wamepewa huo, nao watalikanyaga jiji takatifu chini ya miguu kwa miezi arobaini na miwili. 3 Nami hakika nitasababisha mashahidi wangu wawili watoe unabii siku elfu moja mia mbili na sitini wakiwa wamevaa nguo ya gunia.” 4 Hao wafananishwa na ile mizeituni miwili na vile vinara vya taa viwili nao wamesimama mbele ya Bwana wa dunia.
5 Na yeyote akitaka kuwadhuru, moto watoka katika vinywa vyao na kumeza maadui wao; na ikitukia yeyote atake kuwadhuru, lazima auawe kwa namna hii. 6 Hawa wana mamlaka ya kufunga mbingu ili kwamba mvua yoyote isinye siku za kutoa kwao unabii, nao wana mamlaka juu ya maji ili kuyageuza yawe damu na kuipiga dunia kwa kila namna ya tauni mara nyingi kadiri watakavyo.
7 Na wakiisha kumaliza kutoa ushahidi wao, hayawani-mwitu apandaye kutoka katika abiso atafanya vita pamoja nao na kuwashinda na kuwaua. 8 Na maiti zao zitakuwa juu ya njia pana ya jiji kubwa ambalo katika maana ya kiroho laitwa Sodoma na Misri, ambako pia Bwana wao alitundikwa mtini. 9 Na wale kati ya vikundi vya watu na makabila na lugha na mataifa watatazama maiti zao kwa siku tatu na nusu, na hawaachi maiti zao zilazwe kaburini. 10 Na wale wanaokaa juu ya dunia washangilia juu yao na kujifurahisha wenyewe, na watapelekeana zawadi, kwa sababu hawa manabii wawili waliwatesa-tesa wale wanaokaa juu ya dunia.
11 Na baada ya siku tatu na nusu roho ya uhai kutoka kwa Mungu ikawaingia, nao wakasimama kwa miguu yao, na hofu kubwa ikawaingia wale waliokuwa wakiwatazama. 12 Nao wakasikia sauti kubwa kutoka mbinguni ikiwaambia: “Pandeni mje huku.” Nao wakapanda kwenda juu kuingia mbinguni katika wingu, na maadui wao wakawatazama. 13 Na katika saa hiyo tetemeko kubwa la dunia likatukia, na sehemu ya kumi ya hilo jiji ikaanguka; na watu elfu saba wakauawa na hilo tetemeko la dunia, na wale wengine wakawa wenye kuogopa na kumpa utukufu Mungu wa mbinguni.
14 Ole wa pili umepita. Tazama! Ole wa tatu unakuja upesi.
15 Na malaika wa saba akapuliza tarumbeta yake. Na sauti kubwa zikatokea mbinguni, zikisema: “Ufalme wa ulimwengu ulipata kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atatawala akiwa mfalme milele na milele.”
16 Na wale wazee ishirini na wanne waliokuwa wameketi juu ya viti vyao vya ufalme mbele ya Mungu wakaanguka kifudifudi na kumwabudu Mungu, 17 wakisema: “Twakushukuru wewe, Yehova Mungu, Mweza-Yote, Uliyeko na uliyekuwako, kwa sababu umechukua nguvu yako kubwa na kuanza kutawala ukiwa mfalme. 18 Lakini mataifa wakawa na hasira ya kisasi, na hasira ya kisasi yako mwenyewe ikaja, na wakati uliowekwa rasmi kwa ajili ya wafu kuhukumiwa, na kuwapa thawabu yao watumwa wako hao manabii na watakatifu na wale wanaohofu jina lako, wadogo na wakubwa, na kuwaleta kwenye uangamizi wale wanaoiangamiza dunia.”
19 Na patakatifu pa hekalu la Mungu palipo katika mbingu pakafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana katika patakatifu pa hekalu lake. Na kukatokea meme na sauti na ngurumo na tetemeko la dunia na mvua kubwa ya mawe.