Alitii Mungu Kuwa Mtawala Kuliko Wanadamu
“Ni lazima sisi tutii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu.”
KARIBU miaka 2,000 iliyopita, maneno hayo ya ujasiri yalisikika katika jumba la baraza la Kiyahudi katika Yerusalemu. Kikundi cha Wakristo wa karne ya kwanza kilikuwa kikiulizwa maulizo na kuhani mkuu Myahudi. Walikuwa wamekamatwa hekaluni wakifundisha mkutano wa watu. Malaika wa Yehova alikuwa amewaamuru waende huko wakahubiri Neno la Mungu. Makuhani hao walikuwa wamewaambia wasifanye hivyo. Wewe ungetii nani katika hali kama hiyo? Wakristo hao hawakuwa na shaka. Wao wangetii Mungu kuwa Mtawala kuliko mwanadamu.—Matendo 5:17-32.
Katika zile karne nyingi ambazo zimepita tangu wakati huo, wengine wamefuata mfano wao wa ujasiri wakati viongozi wa kidini, wenyewe wamekataa kuusikia ukweli kama wale makuhani Wayahudi wa karne ya kwanza, na kujaribu kuzuia wengine wasiusikie. (Mathayo 23:13) Mwanzoni mwa karne ya 15, John Husa (1371-1415) aliyatumia maneno hayo hayo alipoagizwa asihubiri katika nchi ya kwao Bohemia (sehemu moja ya Chekoslovakia ya kisasa). Yeye aliitambua mamlaka kuu zaidi ya Mungu na Neno Lake katika wakati ambao papa na kanisa walionwa kuwa ndio wakuu kuliko mtu mwingineye yote. Yeye alipataje kuchukua msimamo huo?
Myanzo ya Fundisho la Kibiblia la Hus
John Hus alilelewa na mamaye mjane aliyekuwa mwenye shamba dogo, kwa hiyo kupata elimu kulikuwa kazi ya jasho. Mara nyingi alilazimika kuimba katika makanisa ili ajipatie riziki. Lakini ingawa yeye hakuwa mwenye akili nyingi sana, aliweza kupata elimu kwenye Chuo Kikuu cha Prague na mwishowe akainuka mpaka akawa kasisi mwenye cheo katika chuo kikuu.
Wakati huo, kulikuwa na ugomvi mwingi katika chuo kikuu kati ya Wajeremani na Wacheki. Hus akawa mteteaji wa shughuli za Wacheki, na nguvu zake za uongozi zikaongezeka alipokuwa mhubiri mwenye uthabiti zaidi. Kwa muda fulani kulikuwa kumekuwa na msukosuko na mazungumzo juu ya mambo mengi yaliyofanywa vibaya katika Kanisa Katoliki la Roma. Nao uliongezwa sana na mweneo wa maandishi ya John Wycliffe aliyekuwa Mwingereza mwenye kupindua mambo ya kidini. Ile hatua iliyochukuliwa kule Bohemia haikuanzishwa na matukio yaliyotendeka Uingereza; bali, ilitukia wakati mmoja na hayo. John Hus alijikuta akiwa amevutiwa na maandishi ya Wycliffe, hasa kile kichapo On Truth of Holy Scriptures, alichokipata mwaka 1407.
Lakini, alipingwa na Askofu Mkuu Zbynek wa Prague, ambaye hakukubaliana na mahubiri ya Hus na akateketeza hadharani mengi ya maandishi ya Wycliffe katika mwaka 1410. Ndipo Zbynek alipokataza mahubiri yote isipokuwa katika makanisa yenye kutambuliwa, nacho Kikanisa cha Bethlehem ambapo Hus alisimamia hakikuwa kati ya hayo. Hus alikataa kutii katazo la askofu mkuu, akisema kwamba ilimpasa ‘kutii Mungu kuliko wanadamu katika mambo yanayohitajiwa kabisa kwa ajili ya wokovu.’ Yeye alimsihi papa, naye askofu mkuu akamwondoa katika ushirika. Lakini Hus hakuyumba-yumba, kwa maana aliona kwamba ufahamu wake mkubwa zaidi ulikuwa umeinoa dhamiri yake na kuifanya iwe nyepesi zaidi kuitikia mafundisho ya Biblia. Yeye alisema wazi hivi: “Huenda mwanadamu akasema uwongo, lakini Mungu hasemi uwongo,” hivyo akiyarudia maneno ya mtume Paulo kwa Waroma. (Warumi 3:4) Mfalme Wenceslas alitetea hatua ya mapinduzi ya Hus, na mwishowe Zbynek akatoroka nchi hiyo, na muda mfupi baadaye akafa.
Upinzani kwa Hus ulitokea tena alipolaumu shughuli ya kivita dhidi ya mfalme wa Naples na kufunua wazi kwamba watu walikuwa wakiuziwa msamaha kwa matendo yaliyohusiana na shughuli hiyo, hivyo akaharibu njia za mapadri za kupata pesa. Masamaha hayo yaliwezesha mtu apate ondoleo la adhabu ya muda kwa kulipa pesa. Ili kuepuka kuleta matatizo mjini, Hus aliondoka Prague awe katika uhamisho wa muda mashambani. Akiwa huko mwaka 1413 alikiandika kichapo On Simony, ambacho kilifunua kwamba mapadri walipenda pesa na kutaka waungwe mkono na wakuu wa kilimwengu. Hapo tena, mamlaka ya Hus ilikuwa katika Neno la Mungu, akisema: “Kila Mkristo mwaminifu anapaswa kuwa na nia ya kwamba hatashika jambo lo lote lililo kinyume cha Maandiko Matakatifu.”
Hus aliandika pia kitabu chenye kichwa De Ecclesia (Kuhusu Kanisa). Ndani yacho aliweka mapendekezo kadha, moja la hayo likisema hivi: “Kwamba Petro hakuwa kamwe, wala siye, kichwa cha Kanisa.” Aliona kwamba ile mistari mikuu ya Mathayo 16:15-18 ilithibitisha waziwazi kwamba Yesu Kristo ndiye msingi wa kichwa cha Kanisa, ambalo ndilo mwili mzima wa waamini walioitwa. Kwa hiyo sheria ya Kristo iliyo katika Neno la Mungu ndiyo kuu zaidi wala si ile ya Papa. Bali, upapa ulianzishwa na mamlaka ya Roma ya kikoloni,
Ushuhuda Mbele ya Baraza la Constance
Kanisa Katoliki lilishindwa kuendelea kuvumilia jinsi Hus alivyofunua makosa yalo na basi walimwita akapate adhabu ya maoni yake mbele ya Baraza la Constance, lililofanywa kuanzia mwaka 1414 mpaka 1418 karibu na Ziwa Constance.b Ndugu ya Mfalme, Maliki Sigismund, ndiye aliyemwingiza katika mtego wa kuhudhuria, kwa kumwahidi kwamba angekuwa salama salimini, kumbe ikaonekana upesi huo ulikuwa uwongo. Muda mfupi baada ya kufika kwake alikamatwa, lakini yeye akaendelea kupinga mamlaka ya papa na hata ya baraza hilo.
Baraza lilipomwita Hus atangue mawazo na mafundisho yake, yeye alijibu kwamba angefurahi kufanya hivyo akithibitishwa na Maandiko kuwa mwenye makosa, kulingana na 2 Timotheo 3:14-16. Hus aliona kwamba dhamiri yake ingemlaumu sikuzote kama angesingizia kuwa ameyatangua maneno yake na kumbe sivyo. Alitangaza hivi: “Sikuzote mimi nimetaka kwamba nithibitishiwe fundisho lililo bora kutokana na Maandiko, na hapo ndipo ningekuwa tayari sana kuyatangua maneno yangu.” Ijapokuwa yeye alitokeza mwito wa ushindani kwamba mshiriki aliye mdogo zaidi katika baraza hilo amwonyeshe kosa lake kutokana na Neno la Mungu lenyewe, alishtakiwa kuwa mzushi wa kidini mwenye shingo ngumu naye akarudishwa gerezani bila mazungumzo yo yote kutokana na Biblia.
Siku ya Julai 6, 1415 Hus alishtakiwa rasmi katika kathedro ya Constance. Hakuruhusiwa kujibu wakati mashtaka dhidi yake yalipokuwa yakisomwa. Ndipo alipovuliwa upadre wake hadharani, huku maandishi yake yakiteketezwa katika ua wa kanisa. Alielekezwa kwenye uwanja mmoja katika viunga vya mji, na huko akateketezwa kwa moto akiwa kwenye mti. Majivu yake yalikusanywa yakatupwa ndani ya Mto Rhine, ili kuzuia mtu ye yote asiweke mabaki ya mfia-imani huyo awe akimkumbuka. Kwa sababu yeye alikuwa amekuwa na uhusiano wa karibu pamoja na John Wycliffe, baraza hilo lilimshtaki pia mpinduzi huyo wa mambo ya kidini—aliyekuwa amekwisha kufa—wakaagiza maiti yake ifukuliwe na kuteketezwa kwa moto kisha majivu yake yatupwe-tupwe ndani ya Mto Swift katika Uingereza. Baadaye, mfuasi wa Hus aliye mashuhuri zaidi, Jerome wa Prague, aliteketezwa pia akiwa kwenye mti.
Mambo Yaliyotimizwa na Hus
Katika kipindi hicho, Hus alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kuthubutu kupinga mamlaka ya papa na hata ya baraza la kanisa na kuikubali mamlaka kubwa zaidi ya Maandiko badala ya ile ya hao wengine. Hivyo yeye alianzisha hatua za kutetea haki za mtu mwenyewe, uhuru wa dhamiri na wa kusema.
Miaka zaidi ya mia moja baadaye, Martin Lutheri katika Ujeremani alishtakiwa juu ya kuyarudia makosa ya Wycliffe na Hus. Kwa uhakika, Lutheri alikuwa na maoni yale yale ya msingi kama Hus aliposema hivi: “Mimi nisiposhtakiwa na Maandiko na sababu yenyewe kuonekana wazi—sikubali mamlaka ya mapapa wala mabaraza ya kanisa, kwa maana yamepingana-pingana—dhamiri yangu inaongozwa kabisa na Neno la Mungu.” Labda hiyo ndiyo sababu alisema: “Sisi sote ni Wahusi bila kujua.”
Walilofanya Hus, Wycliffe, na Lutheri ni kufufua mengi ya mafundisho ya Wakristo wa kwanza. Bila shaka, wao hawakukamilisha kufanya hivyo kwa sababu haikuwa rahisi siku hizo kuondosha giza lililokuwa limekuwapo kwa karne nyingi. Hata hivyo wote walikubaliana jambo moja la maana: Neno la Mungu lilipasa kuwa kwanza, hata wanadamu wawe wana maoni gani. Wakristo wa kwanza walishikilia maoni ayo hayo yenye nuru kwa sababu walikuwa wamefundishwa na Bwana-mkubwa wao, Yesu Kristo, mwenyewe.—Yohana 17:17; 18:37.
Leo, ni lazima wakristo wachukue msimamo uo huo. Sisi tuna mambo mengi ya kutufaidi kuliko yale ya karne hizo za kwanza. Jambo moja ni kwamba, Biblia inapatikana kwa urahisi katika lugha zilizo nyingi. Pili, katika hizi siku za mwisho roho takatifu imeongoza watu wenye kuitikia wapate ufahamu mkubwa zaidi wa Biblia. Je, wewe umeukubali ufahamu huo? Ikiwa ndivyo, hutasita-sita kuifuata pia kanuni ambayo John Hus aliiga bila ugeugeu. Leo, hesabu kubwa zaidi ya watu kuliko wakati mwinginewo wote katika historia wanaishi kwa kufuata maneno hayo ya mitume: “Ni lazima sisi tutii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu.”—Matendo 5:29, NW.
[Maelezo ya Chini]
a Nyakati nyingine mwendelezo la jina hilo ni Huss.
b Baraza ni mkutano wa maaskofu na viongozi wengine wa Kanisa Katoliki ili kufikiria na kupokeza maamuzi juu ya mafundisho, nidhamu, na mambo mengine. Katika muda wote wa historia kulikuwa na mabaraza kadha ya namna hiyo ambayo yanatambuliwa na Kanisa Katoliki la Roma.
[Picha katika ukurasa wa 29]
John Hus
[Picha katika ukurasa wa 31]
Biblia za Kicheki, kama vile chapa ya mwaka 1579 iliyoonyeshwa juu, zinathaminiwa sana na wakusanyaji leo. John Hus aliteketezwa akiwa kwenye mti kwa sababu alithamini yaliyosemwa na Biblia kuliko maneno ya mwanadamu