Waroma
11 Basi, nauliza, Mungu hakuwakataa watu wake, sivyo? Hilo lisitukie kamwe! Kwa maana mimi pia ni Mwisraeli, wa mbegu ya Abrahamu, wa kabila la Benyamini. 2 Mungu hakuwakataa watu wake, aliowatambua kwanza. Kwani, je, hamjui lisemavyo Andiko kuhusiana na Eliya, yeye aombapo Mungu dhidi ya Israeli? 3 “Yehova, wamewaua manabii wako, wamechimbua madhabahu zako, nami nimeachwa peke yangu, nao wanaitafuta nafsi yangu.” 4 Lakini, hilo tamko la kimungu lamwambia nini? “Nimeacha wanaume elfu saba wasalie kwa ajili yangu mwenyewe, watu ambao hawakukunjia Baali goti.” 5 Kwa hiyo, kwa njia hiyo katika majira yaliyopo kumetokea pia mabaki kulingana na kuchaguliwa ambako ni kwa sababu ya fadhili isiyostahiliwa. 6 Basi ikiwa ni kwa fadhili isiyostahiliwa, si tena kwa sababu ya kazi; kama sivyo, fadhili isiyostahiliwa haithibitiki tena kuwa fadhili isiyostahiliwa.
7 Nini, basi? Jambo lilelile analotafuta sana Israeli kwa bidii yeye hakulipata, lakini wale waliochaguliwa walilipata. Wale wengine walifanya hisia zao kuwa sugu; 8 kama vile imeandikwa: “Mungu amewapa wao roho ya usingizi mzito, amewapa macho ili wasione na masikio ili wasisikie, hadi siku hiihii.” 9 Pia, Daudi asema: “Acha meza yao iwe kwao kinaso na mtego na pingamizi lenye kukwaza na malipo; 10 acha macho yao yawe yenye giza ili wasione, na sikuzote wainamishe mgongo wao.”
11 Kwa hiyo nauliza, Je, walijikwaa hivi kwamba wakaanguka kabisa? Hilo lisitukie kamwe! Lakini kwa hatua yao yenye kosa kuna wokovu kwa watu wa mataifa, kuwachochea wao kwenye wivu. 12 Sasa ikiwa hatua yao yenye kosa humaanisha utajiri kwa ulimwengu, na kupungua kwao kwamaanisha utajiri kwa watu wa mataifa, idadi yao kamili itamaanisha hivyo zaidi sana kama nini!
13 Sasa nasema nanyi mlio watu wa mataifa. Kwa maana kama nilivyo, kwa kweli, mtume kwa mataifa, naitukuza huduma yangu, 14 ili labda kwa njia fulani nipate kuchochea kwenye wivu wale ambao ni mwili wangu mwenyewe na kuokoa baadhi yao kutoka miongoni mwao. 15 Kwa maana ikiwa kutupiliwa mbali kwao humaanisha upatanisho kwa ulimwengu, kupokewa kwao kutamaanisha nini ila uhai kutoka kwa wafu? 16 Zaidi, ikiwa hiyo sehemu ichukuliwayo kuwa matunda ya kwanza ni takatifu, donge liko hivyo pia; na ikiwa mzizi ni mtakatifu, matawi yako hivyo pia.
17 Hata hivyo, ikiwa baadhi ya matawi yalikatwa lakini wewe, ujapokuwa mzeituni wa mwitu, ulipandikizwa miongoni mwayo na kuwa mshiriki wa mzizi wa unono wa mzeituni, 18 usiwe ukichachawa juu ya hayo matawi. Ingawa hivyo, ikiwa unachachawa juu yayo, si wewe uuchukuaye mzizi, bali mzizi hukuchukua wewe. 19 Basi, wewe utasema: “Matawi yalikatwa ili mimi nipate kupandikizwa.” 20 Vema! Kwa sababu ya ukosefu wayo wa imani yalikatwa, lakini wewe umesimama kwa imani. Koma kuwa na mawazo yaliyoinuka sana, bali uwe katika hofu. 21 Kwa maana ikiwa Mungu hakuacha matawi ya asili, wala hatakuacha wewe. 22 Kwa hiyo, ona fadhili na ukali wa Mungu. Kuelekea wale walioanguka kuna ukali, lakini kuelekea wewe kuna fadhili ya Mungu, mradi wakaa katika fadhili yake; ama sivyo, wewe pia utapogolewa. 23 Wao pia, ikiwa hawakai katika ukosefu wao wa imani, watapandikizwa; kwa maana Mungu aweza kuwapandikiza wao tena. 24 Kwa maana ikiwa wewe ulikatwa kutoka kwenye mti wa zeituni ulio wa mwitu kwa asili na kupandikizwa kinyume cha asili katika mti wa zeituni wa bustanini, si afadhali zaidi kwamba hawa walio wa asili watapandikizwa kuingia katika mti wao wenyewe wa zeituni!
25 Kwa maana sitaki nyinyi, akina ndugu, mwe wasio na ujuzi juu ya siri takatifu hii, kusudi msiwe wenye busara machoni penu wenyewe: kwamba kutiwa uzito kwa hisi kumewatukia Israeli kwa sehemu mpaka idadi kamili ya watu wa mataifa iwe imeingia, 26 na kwa namna hii Israeli wote wataokolewa. Kama vile imeandikwa: “Mkombozi atakuja kutoka Zayoni na kugeuzia mbali mazoea ya kutomwogopa Mungu yatoke kwa Yakobo. 27 Na hili ndilo agano kwa upande wangu pamoja nao, niondoleapo mbali dhambi zao.” 28 Kweli, kuhusu habari njema wao ni maadui kwa ajili yenu, lakini kuhusiana na kuchagua [kwa Mungu] wao ni wapendwa kwa ajili ya baba zao wa zamani. 29 Kwa maana zawadi na wito wa Mungu si mambo ambayo yeye atajutia. 30 Kwa maana kama vile nyinyi wakati mmoja mlivyokuwa hamtii Mungu lakini sasa mmeonyeshwa rehema kwa sababu ya kutotii kwao, 31 ndivyo pia hawa sasa wamekuwa wasiotii ikitokeza rehema kwenu, ili wao wenyewe pia wapate kuonyeshwa rehema sasa. 32 Kwa maana Mungu amewafunga wao wote pamoja katika kutotii, ili apate kuwaonyesha wao wote rehema.
33 Lo! kina cha utajiri wa Mungu na hekima na ujuzi! Jinsi hukumu zake zisivyotafutikana na njia zake zapita uwezo wa kufuatilia! 34 Kwa maana “ni nani amekuja kuijua akili ya Yehova, au ni nani amekuwa mshauri wake?” 35 Au, “Ni nani amempa yeye kwanza, hivi kwamba lazima kirudishwe kwake?” 36 Kwa sababu vitu vyote ni kutoka kwake na kwa yeye na kwa ajili yake. Kwake kuwe utukufu milele. Ameni.