Waroma
12 Kwa sababu hiyo nawasihi sana nyinyi kwa huruma za Mungu, akina ndugu, mtoe miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, yenye kukubalika kwa Mungu, utumishi mtakatifu pamoja na nguvu zenu za kufikiri kuzuri. 2 Na komeni kufanyizwa kulingana na mtindo wa mfumo huu wa mambo, bali mgeuzwe umbo kwa kufanya upya akili yenu, ili mpate kujithibitishia wenyewe mapenzi ya Mungu yaliyo mema na yenye kukubalika na makamilifu.
3 Kwa maana kupitia fadhili isiyostahiliwa niliyopewa naambia kila mtu huko miongoni mwenu asijifikirie mwenyewe zaidi kuliko ilivyo lazima kufikiri; bali afikiri ili awe na akili timamu, kila mmoja kama vile Mungu amemgawia kipimo cha imani. 4 Kwa maana kama vile tulivyo na viungo vingi katika mwili mmoja, lakini si viungo vyote vyenye kazi ileile, 5 ndivyo sisi, tujapokuwa wengi, tulivyo mwili mmoja katika muungano na Kristo, lakini viungo ambavyo kila kimoja ni cha kile kingine. 6 Basi, kwa kuwa tuna zawadi zinazotofautiana kulingana na fadhili isiyostahiliwa tuliyopewa, kama ni unabii, acheni sisi tutoe unabii kulingana na imani tuliyogawiwa; 7 au huduma, acheni tuwe kwenye huduma hii; au yeye afundishaye, acheni awe kwenye kufundisha kwake; 8 au yeye ahimizaye kwa bidii, acheni ajishughulishe katika himizo lake la bidii; yeye agawaye, acheni afanye hilo kwa ukarimu; yeye asimamiaye, acheni afanye hilo katika bidii halisi; yeye aonyeshaye rehema, acheni afanye hilo kwa uchangamfu.
9 Acheni upendo wenu uwe bila unafiki. Kirihini lililo ovu, ambataneni na lililo jema. 10 Katika upendo wa kidugu iweni na shauku nyororo kwa mtu na mwenzake. Katika kuonyeshana heshima iweni wenye kuongoza. 11 Msicheze-cheze katika shughuli yenu. Iweni wenye kuwaka roho. Tumikieni Yehova kama watumwa. 12 Shangilieni katika tumaini. Vumilieni chini ya dhiki. Dumuni katika sala. 13 Shirikini pamoja na watakatifu kulingana na mahitaji yao. Fuateni mwendo wa ukaribishaji-wageni. 14 Fulizeni kubariki wale ambao hunyanyasa; iweni wenye kubariki wala msiwe wenye kulaani. 15 Shangilieni pamoja na watu washangiliao; toeni machozi pamoja na watu watoao machozi. 16 Iweni na nia ya jinsi ileile kuelekea wengine kama ilivyo kwenu wenyewe; msiwe mkiweka akili juu ya mambo yaliyoinuka, bali mwe mkiongozwa na mambo yaliyo ya hali ya chini. Msipate kuwa wenye busara machoni penu wenyewe.
17 Msirudishe ovu kwa ovu kwa yeyote. Andaeni mambo bora mbele ya macho ya watu wote. 18 Ikiwezekana, kwa kadiri itegemeavyo nyinyi, iweni wenye kufanya amani na watu wote. 19 Wapendwa, msijilipizie kisasi wenyewe bali iachieni nafasi hasira ya kisasi; kwa maana imeandikwa: “Kisasi ni changu; hakika mimi nitalipa, asema Yehova.” 20 Lakini, “ikiwa adui yako ana njaa, mlishe; ikiwa ana kiu, mpe kitu cha kunywa; kwa maana kwa kufanya hilo utarundika makaa-mawe yenye moto juu ya kichwa chake.” 21 Usijiache mwenyewe ushindwe na lililo ovu, bali fuliza kushinda lililo ovu kwa lililo jema.