1 Yohana
5 Kila mtu anayeamini kwamba Yesu ndiye Kristo amezaliwa kutokana na Mungu, na kila mtu ambaye hupenda yule ambaye alisababisha kuzaliwa hupenda yeye ambaye amezaliwa kutokana na huyo. 2 Kwa hili sisi twapata ujuzi kwamba tunapenda watoto wa Mungu, wakati tunapompenda Mungu na kufanya amri zake. 3 Kwa maana hivi ndivyo kumpenda Mungu humaanisha, kwamba tushike amri zake; na bado amri zake si zenye kulemea, 4 kwa sababu kila kitu ambacho kimezaliwa kutokana na Mungu hushinda ulimwengu. Na huu ndio ushindi ambao umeshinda ulimwengu, imani yetu.
5 Ni nani ambaye hushinda ulimwengu ila yeye ambaye ana imani kwamba Yesu ndiye Mwana wa Mungu? 6 Huyu ndiye ambaye alikuja kwa njia ya maji na damu, Yesu Kristo; si kwa maji tu, bali kwa maji na kwa damu. Na roho ndiyo ile inayotoa ushahidi, kwa sababu roho ndiyo kweli. 7 Kwa maana kuna vitoaji ushahidi vitatu, 8 roho na maji na damu, na hivyo vitatu viko katika upatano.
9 Ikiwa twapokea ushahidi ambao wanadamu hutoa, ushahidi ambao Mungu hutoa ni mkubwa zaidi, kwa sababu huu ndio ushahidi ambao Mungu hutoa, jambo la kwamba ametoa ushahidi kuhusu Mwana wake. 10 Mtu anayeweka imani yake katika Mwana wa Mungu ana ushahidi ukiwa umetolewa katika kisa chake mwenyewe. Mtu anayekuwa hana imani katika Mungu amemfanya yeye mwongo, kwa sababu hajaweka imani yake katika ushahidi ambao umetolewa, ambao Mungu akiwa shahidi ametoa kuhusu Mwana wake. 11 Na huu ndio ushahidi ambao umetolewa, kwamba Mungu alitupa sisi uhai udumuo milele, na uhai huu umo katika Mwana wake. 12 Yeye ambaye ana Mwana ana uhai huu; yeye ambaye hana Mwana wa Mungu hana uhai huu.
13 Nawaandikia nyinyi mambo haya ili mpate kujua kwamba nyinyi mnao uhai udumuo milele, nyinyi ambao mwaweka imani yenu katika jina la Mwana wa Mungu. 14 Na huu ndio uhakika ambao tunao kumwelekea yeye, kwamba, hata iwe ni nini ambacho twaomba kulingana na mapenzi yake, yeye hutusikia. 15 Zaidi, ikiwa twajua yeye hutusikia kwa habari ya chochote kile tunachoomba, twajua tutakuwa na mambo yaliyoombwa kwa kuwa tumeyaomba kwake.
16 Yeyote akiona ndugu yake anafanya dhambi, dhambi ambayo haipasishi kifo, ataomba, na yeye atampa uhai, ndiyo, kwa wale ambao hawafanyi dhambi hata kupasisha kifo. Kuna dhambi ambayo yapasisha kifo. Ni kuhusu dhambi hiyo kwamba simwambii afanye ombi. 17 Ukosefu wote wa uadilifu ni dhambi; na bado kuna dhambi ambayo haipasishi kifo.
18 Sisi twajua kwamba kila mtu ambaye amezaliwa kutokana na Mungu hazoei dhambi, lakini Yule ambaye amezaliwa kutokana na Mungu humlinda yeye, na mwovu hakazi mshiko wake juu yake. 19 Sisi twajua twatokana na Mungu, lakini ulimwengu mzima unakaa katika nguvu ya mwovu. 20 Lakini twajua kwamba Mwana wa Mungu amekuja, na yeye ametupa sisi uwezo wa akili ili tupate ujuzi juu ya aliye wa kweli. Na sisi tumo katika muungano na aliye wa kweli, kwa njia ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli na uhai udumuo milele. 21 Watoto wadogo, jilindeni wenyewe na sanamu.