Yuda
Barua ya Yuda
1 Yuda, mtumwa wa Yesu Kristo, lakini ndugu ya Yakobo, kwa walioitwa ambao ni wapendwa katika uhusiano pamoja na Mungu Baba na waliohifadhiwa kwa ajili ya Yesu Kristo:
2 Rehema na amani na upendo na ziongezwe kwenu.
3 Wapendwa, ingawa nilikuwa nikifanya kila jitihada kuwaandikia nyinyi juu ya wokovu ambao sisi twashika kwa shirika, niliona ni lazima niwaandikie ili kuwahimiza kwa bidii mfanye pigano kali kwa ajili ya imani ambayo ilikabidhiwa mara moja kwa wakati wote kwa watakatifu. 4 Sababu yangu ni kwamba watu fulani wamepenyeza ndani ambao zamani za kale wamewekwa rasmi na Maandiko kwa hukumu hii, watu wasiomwogopa Mungu, wakigeuza fadhili isiyostahiliwa ya Mungu wetu kuwa sababu ya kujitetea kwa ajili ya mwenendo mlegevu na kuthibitika kuwa wasio wa kweli kwa Mmiliki na Bwana wetu pekee, Yesu Kristo.
5 Nataka kuwakumbusha nyinyi, ijapokuwa kujua kwenu mambo yote mara moja kwa wakati wote, kwamba Yehova, ijapokuwa aliokoa watu kutoka nchi ya Misri, baadaye aliangamiza wale wasioonyesha imani. 6 Na malaika ambao hawakutunza cheo chao cha awali bali wakaachilia mbali mahali pao wenyewe pa kukaa penye kufaa amewaweka akiba wakiwa na vifungo vya milele chini ya giza zito kwa hukumu ya siku kubwa. 7 Ndivyo pia Sodoma na Gomora na majiji yaliyo kando-kando yayo, baada ya hayo kuwa yamefanya uasherati kwa kuzidi mno na kutoka kwenda kufuatia mwili kwa ajili ya utumizi usio wa asili, katika namna ileile kama hao waliotangulia kutajwa, yamewekwa mbele yetu kuwa kielelezo cha kuonya kwa kupatwa na adhabu ya kihukumu ya moto udumuo milele.
8 Kwa namna kama hiyo, ingawaje, watu hawa, pia, wakijitia mno katika ndoto, wanautia mwili unajisi na kupuuza ubwana na kusema kwa maneno yenye kuudhi juu ya watukufu. 9 Lakini wakati Mikaeli malaika mkuu alipokuwa na tofauti pamoja na Ibilisi na alikuwa akibishana juu ya mwili wa Musa, yeye hakuthubutu kuleta hukumu dhidi yake katika maneno yenye kuudhi, bali alisema: “Yehova na akukemee wewe.” 10 Lakini watu hawa wanasema kwa maneno yenye kuudhi juu ya mambo yale yote ambayo kwa kweli hawayajui; lakini mambo yale yote ambayo wao wayaelewa kiasili kama wanyama wasiofikiri, katika mambo haya wanaendelea kujifisidi wenyewe.
11 Ole wao, kwa sababu wamekwenda katika pito la Kaini, na wametimua mbio kali kuingia katika mwendo wenye kosa wa Balaamu kwa ajili ya thawabu, nao wameangamia katika maongezi ya uasi ya Kora! 12 Hao ndio miamba iliyofichwa chini ya maji katika karamu zenu za upendo huku wakila karamu pamoja nanyi, wachungaji ambao hujilisha wenyewe bila hofu; mawingu yasiyo na maji ambayo yachukuliwa na pepo huku na huku; miti katika majira ya mpukutiko yaliyosonga, lakini isiyo na matunda, ikiisha kufa mara mbili, ikiisha kung’olewa na mizizi; 13 mawimbi yasiyotulia ya bahari ambayo yatoa povu la visababishi vyao wenyewe vya aibu; nyota zisizo na kipito kamili cha mwendo uliowekwa, ambazo kwa ajili yazo weusi wa giza wasimama ukiwa umewekwa akiba milele.
14 Ndiyo, Enoki, wa saba katika mstari kutoka Adamu, alitoa unabii pia kuwahusu, wakati aliposema: “Tazama! Yehova alikuja na makumi ya maelfu yake watakatifu, 15 kutekeleza hukumu dhidi ya wote, na kuwathibitisha ni wenye hatia wote wasiomwogopa Mungu kuhusu vitendo vyao vyote vya kutomwogopa Mungu ambavyo walitenda kwa njia ya kutomwogopa Mungu, na kuhusu mambo yote ya kushtua ambayo watenda-dhambi wasiomwogopa Mungu walisema dhidi yake.”
16 Watu hawa ni wanung’unikaji, walalamikaji juu ya fungu lao maishani, wakiendelea kulingana na tamaa zao wenyewe, na vinywa vyao husema mambo ya kujivimbisha, huku wakisifu kwa kustaajabia watu mashuhuri kwa ajili ya manufaa yao wenyewe.
17 Kwa habari yenu, wapendwa, kumbukeni semi ambazo zilikuwa zimesemwa hapo awali na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo, 18 jinsi walivyokuwa na kawaida ya kuwaambia: “Katika wakati wa mwisho kutakuwako wadhihaki, wakiendelea kulingana na tamaa zao wenyewe kwa ajili ya mambo ya kutomwogopa Mungu.” 19 Hao ndio wale ambao hufanya mitengano, watu wa kinyama, wakiwa hawana ukiroho. 20 Lakini nyinyi, wapendwa, kwa kujijenga wenyewe juu ya imani yenu takatifu zaidi sana, na kusali mkiwa na roho takatifu, 21 jitunzeni wenyewe katika upendo wa Mungu, huku mkingojea rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo kwa tazamio la uhai udumuo milele. 22 Pia, endeleeni kuwaonyesha rehema baadhi ya walio na shaka; 23 waokoeni kwa kuwanyakua kutoka katika moto. Lakini endeleeni kuonyesha wengine rehema, mkifanya hivyo kwa hofu, huku mkilichukia hata vazi la ndani ambalo limetiwa vidoa na mwili.
24 Sasa kwa yeye ambaye aweza kuwalinda nyinyi msijikwae na kuwaweka mwe bila waa mbele ya utukufu wake kwa shangwe kubwa, 25 kwa Mungu pekee aliye Mwokozi wetu kupitia Yesu Kristo Bwana wetu, uwe utukufu, ukuu, uweza na mamlaka kwa umilele wote uliopita na sasa na hadi ndani ya umilele wote. Ameni.