Waebrania
12 Kwa hiyo, basi, kwa sababu tuna wingu kubwa hivyo la mashahidi likituzingira, acheni sisi pia tuondoe kila uzito na dhambi ambayo hututatanisha kwa urahisi, na acheni tukimbie kwa uvumilivu shindano la mbio lililowekwa mbele yetu, 2 tumkaziapo macho Wakili Mkuu na Mkamilishaji wa imani yetu, Yesu. Kwa ajili ya shangwe iliyowekwa mbele yake alivumilia mti wa mateso, akidharau aibu, na ameketi kwenye mkono wa kuume wa kiti cha ufalme cha Mungu. 3 Kwa kweli, fikirieni sana yeye ambaye amevumilia maongezi yaliyo kinyume ya namna hiyo yenye kufanywa na watenda-dhambi dhidi ya masilahi yao wenyewe, ili nyinyi msipate kuchoka na kuzimia katika nafsi zenu.
4 Katika kuendelea na shindano lenu dhidi ya dhambi hiyo bado hamjakinza kamwe hadi damu, 5 bali mmesahau kabisa himizo lenye bidii ambalo lawataja nyinyi kama wana: “Mwana wangu, usipuuze nidhamu kutoka kwa Yehova, wala usizimie wakati usahihishwapo naye; 6 kwa maana ambaye Yehova ampenda humtia nidhamu; kwa kweli, yeye humpiga mijeledi kila mtu ambaye yeye ampokea kuwa mwana.”
7 Ni kwa ajili ya nidhamu nyinyi mnavumilia. Mungu anashughulika nanyi kama na wana. Kwa maana ni mwana gani huyo ambaye baba hamtii nidhamu? 8 Lakini ikiwa nyinyi hamna nidhamu ambayo wote wamekuwa washiriki, nyinyi kwa kweli ni watoto haramu, wala si wana. 9 Zaidi ya hilo, tulikuwa na kawaida ya kuwa na baba waliokuwa wa mwili wetu kututia nidhamu, nasi tulikuwa na kawaida ya kuwapa wao staha. Je, hatutajitiisha wenyewe zaidi sana kwa Baba wa maisha yetu ya kiroho na kuishi? 10 Kwa maana wao kwa siku chache walikuwa na kawaida ya kututia sisi nidhamu kulingana na lile lililoonekana kuwa jema kwao, lakini yeye hufanya hivyo kwa faida yetu ili tupate kushiriki utakatifu wake. 11 Kweli, hakuna nidhamu ionekanayo kwa wakati wa sasa kuwa yenye shangwe, bali yenye kihoro; lakini baadaye kwa wale ambao wamezoezwa nayo hiyo hutoa tunda lenye kufanya amani, yaani, uadilifu.
12 Kwa sababu hiyo inyoosheni mikono ining’iniayo na magoti yaliyodhoofishwa, 13 na fulizeni kufanyia miguu yenu mapito yaliyo manyoofu, ili kilicho kilema kisipate kuteguliwa, bali badala ya hivyo kipate kuponywa. 14 Fuatieni amani pamoja na watu wote, na utakaso ambao bila huo hakuna mtu atakayemwona Bwana, 15 mkilinda kwa uangalifu kwamba yeyote asipate kukosa fadhili isiyostahiliwa ya Mungu; kwamba mzizi wowote wenye sumu usipate kuchipuka na kusababisha taabu na kwamba wengi wasipate kutiwa unajisi na huo; 16 ili kusipate kuwa na mwasherati wala yeyote asiyethamini mambo matakatifu, kama Esau, ambaye kwa kubadilishana na mlo mmoja alitoa haki zake za kuwa mzaliwa wa kwanza. 17 Kwa maana mwajua kwamba baadaye pia alipotaka kurithi baraka alikataliwa, kwa maana, ijapokuwa alitafuta kwa bidii badiliko la nia kwa machozi, hakupata mahali kwa ajili ya hilo.
18 Kwa maana nyinyi hamjakaribia kile kiwezacho kuguswa na ambacho kimewashwa miali kwa moto, na wingu jeusi na giza jeusi na tufani, 19 na mlio wa tarumbeta na sauti ya maneno; sauti ambayo watu walipoisikia waliomba kwa kusihi sana kwamba neno lisiongezwe kwao. 20 Kwa maana hii amri haikuwa yenye kuhimilika kwao: “Na hayawani akigusa mlima, lazima apigwe kwa mawe.” 21 Pia, wonyesho ulikuwa wa kuhofisha sana hivi kwamba Musa akasema: “Mimi ni mwenye hofu na ninatetemeka.” 22 Lakini nyinyi mmekaribia Mlima Zayoni na jiji la Mungu aliye hai, Yerusalemu la kimbingu, na makumi ya maelfu ya malaika, 23 katika kusanyiko kuu, na kutaniko la wazaliwa wa kwanza ambao wameandikwa orodha katika mbingu, na Mungu Hakimu wa wote, na maisha za kiroho za waadilifu ambao wamefanywa wakamilifu, 24 na Yesu mpatanishi wa agano jipya, na damu ya kunyunyiza, ambayo husema kwa njia bora zaidi kuliko damu ya Abeli.
25 Angalieni kwamba hamtoi udhuru kwake anayesema. Kwa maana ikiwa hawakuponyoka waliotoa udhuru kwake aliyekuwa akitoa onyo la kimungu juu ya dunia, ni zaidi sana sisi hatutaponyoka tukigeukia mbali kutoka kwa yeye asemaye kutoka kwenye mbingu. 26 Wakati huo sauti yake iliitikisa dunia, lakini sasa yeye ameahidi, akisema: “Bado mara nyingine tena hakika mimi nitaweka katika msukosuko si dunia tu bali pia mbingu.” 27 Sasa huo usemi “Bado mara nyingine tena” watoa ishara ya kuondolewa kwa vitu vyenye kutikiswa kama vitu ambavyo vimefanywa, ili vitu visivyotikiswa vipate kubaki. 28 Kwa sababu hiyo, kwa kuwa tutapokea ufalme usioweza kutikiswa, acheni sisi tuendelee kuwa na fadhili isiyostahiliwa, ambayo kupitia hiyo twaweza kumtolea Mungu katika njia ya kukubalika utumishi mtakatifu kwa hofu ya kimungu na kicho. 29 Kwa maana Mungu wetu ni moto unaokula kabisa pia.