Waebrania
11 Imani ni taraja lililohakikishwa la mambo yatumainiwayo, wonyesho dhahiri wa mambo halisi ingawa hayaonwi. 2 Kwa maana kwa njia ya imani hiyo wanaume wa nyakati za zamani walitolewa ushahidi.
3 Kwa imani twafahamu kwamba mifumo ya mambo iliwekwa katika utaratibu kwa neno la Mungu, hivi kwamba lile ambalo laonwa limekuja kutokana na mambo yasiyoonekana.
4 Kwa imani Abeli alimtolea Mungu dhabihu ya thamani kubwa zaidi kuliko Kaini, imani ambayo kupitia hiyo alitolewa ushahidi kwamba yeye alikuwa mwadilifu, Mungu akitoa ushahidi kwa habari ya zawadi zake; na kupitia hiyo yeye, ijapokuwa alikufa, bado asema.
5 Kwa imani Enoki alihamishwa ili asione kifo, naye hakupatikana mahali popote kwa sababu Mungu alikuwa amemhamisha; kwa maana kabla ya uhamisho wake alikuwa na ushahidi kwamba alikuwa amempendeza Mungu vema. 6 Zaidi ya hayo, bila imani haiwezekani kumpendeza vema, kwa maana amkaribiaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na kwamba yeye huwa mthawabishaji wa wale wanaomtafuta kwa bidii.
7 Kwa imani Noa, baada ya kupewa onyo la kimungu la mambo yasiyoonwa bado, alionyesha hofu ya kimungu akajenga safina kwa ajili ya kuokoa watu wa nyumbani mwake; na kupitia imani hiyo aliuhukumu ulimwengu kuwa wastahili adhabu, naye akawa mrithi wa uadilifu ulio kulingana na imani.
8 Kwa imani Abrahamu, alipoitwa, alitii kwa kutoka kuingia mahali alipokusudiwa apapokee kuwa urithi; naye akatoka, ijapokuwa asijue ni wapi alikokuwa akienda. 9 Kwa imani yeye alikaa kama mgeni asiye mzalia katika nchi ya ahadi kama katika nchi ya ugenini, na kukaa katika mahema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ileile. 10 Kwa maana alikuwa akingojea jiji lililo na misingi halisi, ambalo mjenzi na mfanyi wa jiji hilo ni Mungu.
11 Kwa imani pia Sara yeye mwenyewe alipokea nguvu ili kuchukua mimba ya mbegu, hata alipokuwa amepita kiwango cha umri, kwa kuwa alimkadiria kuwa mwaminifu yeye aliyekuwa ameahidi. 12 Kwa sababu hiyo pia kutoka kwa mtu mmoja, naye akiwa kana kwamba ni mfu, kulizaliwa watoto kama vile nyota za mbinguni kwa wingi na kama mchanga ulio kando ya bahari, usiohesabika.
13 Katika imani wote hao walikufa, ijapokuwa hawakupata utimizo wa ahadi, bali waliziona kwa mbali na kuzikaribisha na kutangaza hadharani kwamba wao walikuwa watu wasiojulikana na wakaaji wa muda katika nchi. 14 Kwa maana wale wasemao mambo ya namna hiyo hutoa uthibitisho wa kwamba wanatafuta kwa bidii mahali pao wenyewe. 15 Na bado, kama kwa kweli wangalifuliza kukumbuka mahali hapo walipokuwa wametoka, wangalikuwa na fursa ya kurudi. 16 Lakini sasa wanajitahidi kufikilia mahali palipo bora, yaani, pamoja ambapo ni pa mbinguni. Kwa sababu hiyo Mungu haaibiki juu yao, kuitwa akiwa Mungu wao, kwa maana amefanya jiji liwe tayari kwa ajili yao.
17 Kwa imani Abrahamu, alipojaribiwa, ni kana kwamba alimtoa Isaka, na huyo mtu aliyekuwa amezipokea ahadi kwa mteremo akajaribu kutoa mwana wake mzaliwa-pekee, 18 ijapokuwa alikuwa ameambiwa: “Itakayoitwa ‘mbegu yako’ itakuwa kupitia Isaka.” 19 Lakini alihesabu kwamba Mungu alikuwa aweza kumfufua hata kutoka kwa wafu; na kutoka huko alimpokea pia katika njia ya kielezi.
20 Kwa imani pia Isaka alibariki Yakobo na Esau kuhusu mambo yajayo.
21 Kwa imani Yakobo, alipokuwa karibu kufa, alibariki kila mmoja wa wana wa Yosefu na kuabudu akiegemea juu ya fimbo yake.
22 Kwa imani Yosefu, akikaribia mwisho wake, alifanya mtajo wa kule kutoka kwa wana wa Israeli; naye akatoa amri kuhusu mifupa yake.
23 Kwa imani Musa alifichwa kwa miezi mitatu na wazazi wake baada ya kuzaliwa kwake, kwa sababu wao waliona huyo mtoto mchanga alikuwa mzuri nao hawakulihofu agizo la mfalme. 24 Kwa imani Musa, alipokuwa amekua akawa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti ya Farao, 25 akichagua kutendwa vibaya pamoja na watu wa Mungu badala ya kuwa na mfurahio wa muda wa dhambi, 26 kwa sababu alikadiria shutumu la Kristo kuwa utajiri mkubwa zaidi kuliko hazina za Misri; kwa maana alikaza macho kuelekea malipo ya thawabu. 27 Kwa imani aliondoka Misri, lakini bila kuihofu hasira ya mfalme, kwa maana aliendelea akiwa imara kama ambaye anaona Yeye asiyeonekana. 28 Kwa imani alifanya kuwe kusherehekea sikukuu ya kupitwa na kurashiwa kwa damu, ili mwangamizi asipate kuwagusa wazaliwa wao wa kwanza.
29 Kwa imani walipita katika Bahari Nyekundu juu ya nchi kavu, lakini kwa kujasiria hilo Wamisri wakamezwa.
30 Kwa imani kuta za Yeriko zilianguka chini baada ya kuwa zimezungukwa kwa siku saba. 31 Kwa imani Rahabu kahaba hakuangamia pamoja na wale waliotenda kwa kutotii, kwa sababu aliwapokea wapelelezi kwa njia ya kufanya amani.
32 Na ni nini zaidi nitakalosema? Kwa maana wakati utakosekana kwangu nikiendelea kusimulia juu ya Gideoni, Baraki, Samsoni, Yeftha, Daudi na vilevile Samweli na wale manabii wengine, 33 ambao kupitia imani walishinda falme katika pambano, wakatekeleza uadilifu, wakapata ahadi, wakaziba vinywa vya simba, 34 wakazima kani ya moto, wakaponyoka makali ya upanga, kutoka hali dhaifu wakafanywa wenye nguvu, wakawa mashujaa katika vita, wakatimusha majeshi ya watoka-ugenini. 35 Wanawake waliwapokea wafu wao kwa ufufuo; lakini watu wengine waliteswa-teswa kwa sababu walikuwa hawakubali kuachiliwa kwa njia ya fidia fulani, ili wapate kufikia ufufuo bora. 36 Ndiyo, wengine walipokea jaribu lao kwa dhihaka na mapigo kwa mijeledi, kwa kweli, zaidi ya hilo, kwa vifungo na magereza. 37 Walipigwa kwa mawe, walijaribiwa, walikatwa vipande-vipande kwa msumeno, walikufa kwa kuchinjwa kwa upanga, walienda wakizunguka huku na huku katika ngozi za kondoo, katika ngozi za mbuzi, huku wakiwa katika uhitaji, katika dhiki, chini ya kutendwa vibaya; 38 na ulimwengu haukuwafaa. Walizurura huku na huku katika majangwa na milima na mapango na mashimo ya dunia.
39 Na bado wote hawa, ijapokuwa walitolewa ushahidi kupitia imani yao, hawakupata utimizo wa ahadi, 40 kwa kuwa Mungu aliona kimbele kitu fulani bora kwa ajili yetu sisi, ili wasipate kufanywa wakamilifu bila sisi.