Waebrania
10 Kwa kuwa Sheria ina kivuli cha mambo mema yatakayokuja, lakini si kitu chenyewe hasa cha hayo mambo, watu hawawezi kamwe kwa dhabihu zilezile kutoka mwaka hadi mwaka ambazo wao huzitoa kwa kuendelea kuwafanya wakamilifu wale wakaribiao. 2 Kama sivyo, je, dhabihu hazingalikoma kutolewa, kwa sababu wale wanaotoa utumishi mtakatifu waliokuwa wamesafishwa mara moja kwa wakati wote wasingalikuwa na dhamiri ya dhambi tena kamwe? 3 Kinyume cha hilo, kwa dhabihu hizo kuna kukumbusha juu ya dhambi kutoka mwaka hadi mwaka, 4 kwa maana haiwezekani damu ya mafahali na ya mbuzi kuziondolea mbali dhambi.
5 Kwa sababu hiyo wakati yeye ajapo katika ulimwengu asema: “‘Dhabihu na toleo hukutaka, bali ulinitayarishia mwili. 6 Hukukubalia matoleo mazima ya kuchomwa na toleo la dhambi.’ 7 Ndipo nikasema, ‘Tazama! Nimekuja (katika kikuto cha kitabu imeandikwa juu yangu) ili kufanya mapenzi yako, Ee Mungu.’” 8 Baada ya kwanza kusema: “Hukutaka wala hukukubalia dhabihu na matoleo na matoleo mazima ya kuchomwa na toleo la dhambi” —dhabihu zitolewazo kulingana na Sheria— 9 ndipo kwa kweli asema: “Tazama! Nimekuja kufanya mapenzi yako.” Aondolea mbali la kwanza ili apate kusimamisha lililo la pili. 10 Kwa hayo “mapenzi” yasemwayo sisi tumetakaswa kupitia toleo la mwili wa Yesu Kristo mara moja kwa wakati wote.
11 Pia, kila kuhani huenda mahali pa kazi kutoka siku hadi siku kutoa utumishi wa watu wote na kutoa dhabihu zilezile mara nyingi, kwa kuwa hizi haziwezi wakati wowote kamwe kuziondolea mbali dhambi kabisa. 12 Lakini mtu huyu alitoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi daima dawamu na kuketi kwenye mkono wa kuume wa Mungu, 13 tangu wakati huo na kuendelea akingojea mpaka maadui wake wawekwe kama kibago kwa ajili ya miguu yake. 14 Kwa maana ni kwa toleo moja la kidhabihu kwamba yeye amewafanya wale wanaotakaswa wawe wakamilifu daima dawamu. 15 Zaidi ya hayo, roho takatifu pia hutoa ushahidi kwetu, kwa maana baada ya hiyo kuwa imesema: 16 “‘Hili ndilo agano nitakaloagana kuwaelekea baada ya siku hizo,’ asema Yehova. ‘Hakika nitaweka sheria zangu katika mioyo yao, na katika akili zao nitaziandika,’” 17 hiyo husema baadaye: “Nami kwa vyovyote sitakumbuka tena kamwe dhambi zao na vitendo vyao vya kuasi sheria.” 18 Sasa mahali palipo na msamaha wa hizi, hapana tena toleo kwa ajili ya dhambi.
19 Kwa hiyo, akina ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa njia ya kuingia katika mahali patakatifu kwa damu ya Yesu, 20 aliyotuanzishia kisherehe iwe njia mpya na yenye uhai kupitia pazia, yaani, mwili wake, 21 na kwa kuwa tuna kuhani mkubwa juu ya nyumba ya Mungu, 22 acheni tukaribie tukiwa na mioyo ya kweli katika uhakikisho kamili wa imani, mioyo yetu ikiisha kunyunyiziwa kutoka kwenye dhamiri mbovu na miili yetu kuoshwa kwa maji safi. 23 Acheni tushike sana tangazo la hadharani la tumaini letu bila kuyumbayumba, kwa maana yeye ni mwaminifu aliyeahidi. 24 Na acheni tufikiriane ili kuchocheana kwenye upendo na kazi zilizo bora, 25 si kuachilia mbali kukusanyika pamoja sisi wenyewe, kama vile wengine walivyo na desturi, bali kutiana moyo, na zaidi sana hivyo kwa kadiri mwonavyo siku ikikaribia.
26 Kwa maana tukizoea dhambi kwa kusudi baada ya kuwa tumepokea ujuzi sahihi juu ya kweli, hakuna tena dhabihu yoyote iliyoachwa kwa ajili ya dhambi, 27 lakini kuna taraja fulani lenye hofu la hukumu na kuna wivu wenye moto utakaowala kabisa wale walio katika upinzani. 28 Mtu yeyote ambaye ameipuuza sheria ya Musa hufa bila huruma, juu ya ushuhuda wa wawili au watatu. 29 Je, ni adhabu kali zaidi sana jinsi gani, nyinyi mwafikiri, atahesabiwa kuistahili mtu ambaye amekanyaga-kanyaga juu ya Mwana wa Mungu na ambaye ameikadiria kuwa yenye thamani ya kawaida tu damu ya agano ambayo kwayo alitakaswa, na ambaye ameitendea kwa njia mbaya kabisa yenye dharau roho ya fadhili isiyostahiliwa? 30 Kwa maana twamjua yeye aliyesema: “Kisasi ni changu; hakika mimi nitalipa”; na tena: “Yehova atahukumu watu wake.” 31 Ni jambo lenye kuhofisha kuanguka katika mikono ya Mungu aliye hai.
32 Hata hivyo, fulizeni kukumbuka siku za hapo zamani ambazo katika hizo, baada ya nyinyi kutiwa nuru, mlivumilia shindano kubwa chini ya mateso, 33 nyakati fulani mlipokuwa mkifunuliwa wazi kama katika mahali pa michezo kwenye mashutumu na dhiki pia, na nyakati fulani mlipopata kuwa washiriki pamoja na wale waliokuwa wakipatwa na jambo la namna hiyo. 34 Kwa maana mlionyesha kushiriki hisia kwa ajili ya wale walio gerezani na pia kwa shangwe mkakubali kwa uvumilivu kuporwa mali zenu, mkijua nyinyi wenyewe mna miliki bora na yenye kudumu.
35 Kwa hiyo, msitupilie mbali uhuru wenu wa usemi, ulio na thawabu kubwa ya kulipwa. 36 Kwa maana mna uhitaji wa uvumilivu, ili kwamba, baada ya nyinyi kuwa mmefanya mapenzi ya Mungu, mpate kupokea utimizo wa ahadi. 37 Kwa maana bado “muda kidogo sana,” na “yeye anayekuja atawasili na hatakawia.” 38 “Lakini mwadilifu wangu ataishi kwa sababu ya imani,” na, “ikiwa yeye ajikunyata, nafsi yangu haina upendezi katika yeye.” 39 Sasa sisi si namna irudiyo nyuma kwenye uangamivu, bali namna iliyo na imani kuelekea kuhifadhi hai nafsi.