Waebrania
13 Acheni upendo wenu wa kidugu uendelee. 2 Msisahau ukaribishaji-wageni, kwa maana kupitia huo wengine, bila kujulikana kwao wenyewe, waliwapokea malaika. 3 Wawekeni akilini wale walio katika vifungo vya gereza kama kwamba mmefungwa pamoja nao, na wale wanaotendwa vibaya, kwa kuwa nyinyi wenyewe pia bado mko katika mwili. 4 Acheni ndoa iwe yenye kuheshimika miongoni mwa wote, na kitanda cha ndoa kiwe bila kutiwa unajisi, kwa maana Mungu atawahukumu waasherati na wazinzi. 5 Acheni namna yenu ya maisha iwe bila upendo wa fedha, huku nyinyi mkiridhika na vitu vilivyopo. Kwa maana yeye amesema: “Hakika sitakuacha kwa vyovyote wala kukuachilia mbali kwa vyovyote.” 6 Ili kwamba tupate kuwa wenye moyo mkuu na kusema: “Yehova ni msaidiaji wangu; hakika sitaogopa. Mwanadamu aweza kunifanya nini?”
7 Kumbukeni wale ambao wanaongoza miongoni mwenu, ambao wamelisema neno la Mungu kwenu, nanyi mfikiriapo jinsi mwisho wa mwenendo wao upatavyo kuwa, igeni imani yao.
8 Yesu Kristo ni yuleyule jana na leo, na milele.
9 Msichukuliwe na mafundisho ya namna mbalimbali na yaliyo mageni; kwa maana ni vizuri moyo upewe imara kwa fadhili isiyostahiliwa, si kwa vitu vyenye kulika, ambavyo kwavyo wale wajishughulishao wenyewe navyo hawajanufaishwa.
10 Sisi tuna madhabahu ambayo kutoka hiyo wale wafanyao utumishi mtakatifu kwenye hema hawana mamlaka ya kula. 11 Kwa maana miili ya wale wanyama ambao damu yao hupelekwa na kuhani wa cheo cha juu ndani ya mahali patakatifu kwa ajili ya dhambi huchomwa kabisa nje ya kambi. 12 Kwa sababu hiyo Yesu pia, ili apate kuwatakasa watu kwa damu yake mwenyewe, aliteseka nje ya lango. 13 Basi, acheni sisi twende kwake nje ya kambi, tukilichukua shutumu alilolibeba, 14 kwa maana sisi hatuna hapa jiji liendelealo kuwako, bali tunatafuta kwa bidii litakalokuja. 15 Kupitia yeye acheni sikuzote tumtolee Mungu dhabihu ya sifa, yaani, tunda la midomo ambayo hulifanyia jina lake tangazo la hadharani. 16 Zaidi ya hayo, msisahau kule kutenda mema na kule kushiriki vitu pamoja na wengine, kwa maana kwa dhabihu za namna hiyo Mungu hupendezwa vema.
17 Iweni watiifu kwa wale ambao wanaongoza miongoni mwenu na kuwa wenye kunyenyekea, kwa maana wao wanafuliza kulinda juu ya nafsi zenu kama wale watakaotoa hesabu; ili wapate kufanya hili kwa shangwe na si kwa kutweta, kwa maana hili lingekuwa lenye hasara kwenu.
18 Endelezeni sala kwa ajili yetu, kwa maana sisi twaitibari tuna dhamiri yenye kufuata haki, kwa kuwa twataka kujiendesha wenyewe kwa kufuata haki katika mambo yote. 19 Lakini nawahimiza kwa bidii hasa zaidi mfanye hilo, ili nipate kurudishwa kwenu karibuni zaidi.
20 Sasa Mungu wa amani, aliyemleta kutoka kwa wafu mchungaji mkubwa wa kondoo kwa damu ya agano lidumulo milele, Bwana wetu Yesu, 21 na awape nyinyi vifaa kwa kila jambo jema ili kufanya mapenzi yake, akifanya katika sisi kupitia Yesu Kristo lile ambalo linapendeza vema machoni pake; ambaye kwake kuwe utukufu milele na milele. Ameni.
22 Sasa nawahimiza nyinyi kwa bidii, akina ndugu, mhimili neno hili la kitia-moyo, kwa maana mimi, kwa kweli, nimewatungia barua kwa maneno machache. 23 Jueni kwamba ndugu yetu Timotheo ameachiliwa, ambaye, akija karibuni sana, mimi nitawaona nyinyi nikiwa pamoja naye.
24 Wapeni salamu zangu wote wale ambao wanaongoza miongoni mwenu na watakatifu wote. Wale walio katika Italia wawapelekea nyinyi salamu zao.
25 Fadhili isiyostahiliwa iwe pamoja na nyinyi nyote.