2 Petro
Ya Pili ya Petro
1 Simoni Petro, mtumwa na mtume wa Yesu Kristo, kwa wale ambao wamepata imani, yenye kushikiliwa katika pendeleo lililo sawa na letu, kwa uadilifu wa Mungu wetu na Mwokozi Yesu Kristo:
2 Fadhili isiyostahiliwa na amani zipate kuongezwa kwenu kwa ujuzi sahihi juu ya Mungu na juu ya Yesu Bwana wetu, 3 kwa maana nguvu yake ya kimungu imetupa sisi kwa hiari mambo yote ambayo yahusu uhai na ujitoaji-kimungu, kupitia ujuzi sahihi juu ya yeye ambaye alituita kupitia utukufu na wema wa adili. 4 Kupitia mambo haya ametupa sisi kwa hiari ahadi zenye bei na zilizo bora sana, ili kupitia hizi nyinyi mpate kuwa washiriki katika asili ya kimungu, mkiwa mmeponyoka kutoka katika ufisadi ambao umo katika ulimwengu kupitia uchu.
5 Ndiyo, kwa sababu hiihii, mkiitikia kwa kuchanga kwenu jitihada yote yenye bidii, jazeni kwenye imani yenu wema wa adili, kwenye wema wa adili wenu ujuzi, 6 kwenye ujuzi wenu kujidhibiti, kwenye kujidhibiti kwenu uvumilivu, kwenye uvumilivu wenu ujitoaji-kimungu, 7 kwenye ujitoaji-kimungu wenu shauku ya kidugu, kwenye shauku ya kidugu yenu upendo. 8 Kwa maana ikiwa mambo haya yakaa ndani yenu na kufurika, yatawazuia kuwa ama wasiotenda ama wasiozaa matunda kuhusu ujuzi sahihi juu ya Bwana wetu Yesu Kristo.
9 Kwa maana ikiwa mambo hayo hayakai ndani ya yeyote, yeye ni kipofu, akifunga macho yake kwenye nuru, na amekuwa msahaulifu kuhusu kutakaswa kwake kutoka katika dhambi zake za zamani za kale. 10 Kwa sababu hii, akina ndugu, fanyeni hata zaidi yote kabisa mwezayo, mfanye wito na kuchaguliwa kwenu kuwe hakika kwa ajili yenu wenyewe; kwa maana ikiwa mnafuliza kufanya mambo hayo hamtakosa kwa vyovyote. 11 Kwa kweli, hivyo ndivyo mtapewa kwa utajiri mwingilio katika ufalme udumuo milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.
12 Kwa sababu hii nitakuwa sikuzote na mwelekeo kuwakumbusha nyinyi kuhusu mambo haya, ijapokuwa mwayajua hayo na mmewekwa imara katika kweli ambayo imo katika nyinyi. 13 Lakini nafikiria hili kuwa sawa, maadamu nimo katika tabenakulo hii, kuamsha nyinyi kwa njia ya kuwakumbusha, 14 kama ninavyojua kwamba kuondolewa kwa tabenakulo yangu kutakuwa karibuni, kama vile pia Bwana wetu Yesu Kristo alivyotoa ishara kwangu. 15 Kwa hiyo hakika nitafanya yote kabisa niwezayo pia kila wakati ili, baada ya kuondoka kwangu, nyinyi mpate kuweza kujitajia nyinyi wenyewe mambo haya.
16 Sivyo, haikuwa kwa kufuata hadithi zisizo za kweli zilizotungwa kwa usanifu mwingi kwamba tuliwafahamisha nyinyi juu ya nguvu na kuwapo kwa Bwana wetu Yesu Kristo, lakini ilikuwa kwa kupata kuwa mashahidi wa kujionea fahari yake. 17 Kwa maana alipokea kutoka kwa Mungu Baba heshima na utukufu, wakati maneno ya namna hii yalipopelekwa kwake kwa utukufu wenye fahari: “Huyu ni mwana wangu, mpendwa wangu, ambaye mimi mwenyewe nimemkubali.” 18 Ndiyo, maneno haya tuliyasikia yakipelekwa kutoka mbinguni tulipokuwa tungali pamoja naye katika mlima mtakatifu.
19 Kwa sababu hiyo tuna neno la unabii likiwa limefanywa hakika zaidi; na mnafanya vema kulikazia uangalifu kama vile kwa taa yenye kung’aa mahali penye giza, hadi siku ipambazuke na nyota ya mchana izuke, katika mioyo yenu. 20 Kwa maana mwajua hili kwanza, kwamba hakuna unabii wa Andiko uchipukao kutokana na fasiri yoyote ya faragha. 21 Kwa maana unabii haukuletwa wakati wowote kamwe kwa mapenzi ya binadamu, bali wanadamu walisema kutoka kwa Mungu walipokuwa wakichukuliwa na roho takatifu.