1 Yohana
2 Watoto wangu wadogo, nawaandikia nyinyi mambo haya ili msifanye dhambi. Na bado, ikiwa yeyote afanya hasa dhambi, tuna msaidiaji kwa Baba, Yesu Kristo, aliye mwadilifu. 2 Na yeye ni dhabihu yenye kufunika kwa ajili ya dhambi zetu, lakini si kwa ajili ya zetu tu bali pia kwa ajili ya zile za ulimwengu wote. 3 Na kwa hili tuna ujuzi kwamba tumekuja kumjua yeye, yaani, ikiwa twaendelea kushika amri zake. 4 Yeye ambaye husema: “Mimi nimekuja kumjua,” na bado hashiki amri zake, ni mwongo, na kweli haimo katika mtu huyo. 5 Lakini yeyote yule ashikaye hasa neno lake, kwa kweli katika mtu huyu kumpenda Mungu kumefanywa kukamilifu. Kwa hili tuna ujuzi kwamba sisi tumo katika muungano na yeye. 6 Yeye ambaye husema akaa katika muungano na yeye yuko chini ya wajibu yeye mwenyewe pia kuendelea kutembea kama vile huyo alivyotembea.
7 Wapendwa, ninawaandikia nyinyi, si amri mpya, bali amri ya zamani ambayo mmekuwa nayo tangu mwanzo. Amri hii ya zamani ni neno ambalo mlisikia. 8 Tena, ninawaandikia nyinyi amri mpya, uhakika ambao ni kweli katika kisa chake na katika chenu, kwa sababu giza linapitilia mbali na nuru ya kweli tayari inang’aa.
9 Yeye ambaye husema yumo katika nuru na bado huchukia ndugu yake yumo katika giza hata hivi sasa. 10 Yeye ambaye hupenda ndugu yake hukaa katika nuru, na hakuna sababu yoyote ya kukwaza katika kisa chake. 11 Lakini yeye ambaye huchukia ndugu yake yumo katika giza na anatembea katika giza, na hajui ni wapi anaenda, kwa sababu giza limepofusha macho yake.
12 Ninawaandikia nyinyi, watoto wadogo, kwa sababu dhambi zenu zimesamehewa kwa ajili ya jina lake. 13 Ninawaandikia nyinyi, akina baba, kwa sababu mmekuja kujua yeye aliye wa tangu mwanzo. Nawaandikia nyinyi, wanaume vijana, kwa sababu mmemshinda mwovu. Nawaandikia nyinyi, watoto wachanga, kwa sababu mmekuja kumjua Baba. 14 Ninawaandikia nyinyi, akina baba, kwa sababu mmekuja kumjua yeye aliye wa tangu mwanzo. Ninawaandikia nyinyi, wanaume vijana, kwa sababu nyinyi ni wenye nguvu na neno la Mungu hukaa katika nyinyi na mmemshinda mwovu.
15 Msiwe mkipenda ama ulimwengu ama vitu vilivyo katika ulimwengu. Ikiwa yeyote aupenda ulimwengu, kumpenda Baba hakumo katika yeye; 16 kwa sababu kila kitu kilicho katika ulimwengu—tamaa ya mwili na tamaa ya macho na wonyesho wa mtu wa kujivunia njia yake ya kutegemeza maisha—hakitokani na Baba, bali hutokana na ulimwengu. 17 Zaidi ya hilo, ulimwengu unapitilia mbali na ndivyo na tamaa yao, lakini yeye ambaye hufanya mapenzi ya Mungu hudumu milele.
18 Watoto wachanga, ni saa ya mwisho, na, kama vile ambavyo mmesikia kwamba mpinga-Kristo anakuja, hata sasa kumekuja kuwa wapinga-Kristo wengi; uhakika ambao kutokana nao twapata ujuzi kwamba ni saa ya mwisho. 19 Wao walienda kutoka kwetu, lakini hawakuwa wa namna yetu; kwa maana ikiwa wangekuwa wa namna yetu, wangalibaki pamoja na sisi. Lakini wao walitoka kwenda ili ionyeshwe wazi kwamba si wote walio wa namna yetu. 20 Na nyinyi mna utiwa-mafuta kutoka kwa aliye mtakatifu; nyinyi nyote mna ujuzi. 21 Nawaandikia nyinyi, si kwa sababu hamjui kweli, bali kwa sababu mwaijua, na kwa sababu hakuna uwongo wowote utokanao na kweli.
22 Ni nani aliye mwongo ikiwa si yeye ambaye hukana kwamba Yesu ndiye Kristo? Huyu ndiye mpinga-Kristo, yeye ambaye hukana Baba na Mwana. 23 Kila mtu ambaye hukana Mwana hana Baba pia. Yeye ambaye huungama Mwana ana Baba pia. 24 Kwa habari yenu, acheni lile ambalo mmesikia tangu mwanzo likae katika nyinyi. Ikiwa lile ambalo mmesikia tangu mwanzo lakaa katika nyinyi, nyinyi pia mtakaa katika muungano na Mwana na katika muungano na Baba. 25 Zaidi ya hilo, hili ndilo jambo lililoahidiwa ambalo yeye mwenyewe alituahidi, uhai udumuo milele.
26 Mambo haya nawaandikia nyinyi juu ya wale ambao wanajaribu kuwaongoza vibaya. 27 Na kwa habari yenu, utiwa-mafuta ambao mlipokea kutoka kwake hukaa katika nyinyi, na hamhitaji yeyote awe akiwafundisha; lakini, kama vile utiwa-mafuta kutoka kwake unavyowafundisha nyinyi juu ya mambo yote, na ni kweli wala si uwongo, na kama vile huo umewafundisha nyinyi, kaeni katika muungano na yeye. 28 Kwa hiyo sasa, watoto wadogo, kaeni katika muungano na yeye, ili wakati afanywapo dhahiri sisi tuwe na uhuru wa usemi na tusiaibishwe kutoka kwake katika kuwapo kwake. 29 Ikiwa mwajua kwamba yeye ni mwadilifu, mwapata ujuzi kwamba kila mtu ambaye huzoea uadilifu amezaliwa kutokana na yeye.