Luka
8 Upesi baadaye akaanza kusafiri kutoka jiji hadi jiji na kutoka kijiji hadi kijiji, akihubiri na kutangaza habari njema ya ufalme wa Mungu. Na wale kumi na wawili walikuwa pamoja naye, 2 na wanawake fulani waliokuwa wameponywa roho waovu na magonjwa, Maria aitwaye kwa kawaida Magdalene, ambaye roho waovu saba walikuwa wamemtoka, 3 na Yoana mke wa Kuza, mtu mwenye kusimamia wa Herode, na Susana na wanawake wengine wengi, waliokuwa wakiwahudumia kutokana na mali zao.
4 Sasa umati mkubwa ulipokuwa umekusanyika pamoja na wale waliomwendea kutoka jiji baada ya jiji, akasema kwa njia ya kielezi: 5 “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu yake. Basi, alipokuwa akipanda, baadhi ya hizo zikaanguka kando ya barabara zikakanyagwa-kanyagwa, na ndege wa mbinguni wakazila kabisa. 6 Nyinginezo zikaanguka juu ya tungamo-mwamba, na, baada ya kuota, zikakauka kabisa kwa sababu ya kutokuwa na unyevunyevu. 7 Nyinginezo zikaanguka katikati ya miiba, na miiba iliyokua pamoja nazo ikazisonga. 8 Nyinginezo zikaanguka juu ya udongo mzuri, na, baada ya kuota, zikatokeza matunda mara mia.” Alipokuwa akisema mambo hayo, akapaaza sauti: “Acheni yeye aliye na masikio ya kusikiliza, asikilize.”
9 Lakini wanafunzi wake wakaanza kumuuliza kielezi hiki kingeweza kuwa na maana gani. 10 Akasema: “Nyinyi mmeruhusiwa kuzielewa siri takatifu za ufalme wa Mungu, lakini kwa wale wengine zimo kwa vielezi, ili, ingawa wanatazama, wapate kutazama bure na, ingawa wanasikia, wasiipate maana. 11 Basi hicho kielezi chamaanisha hivi: Hizo mbegu ni neno la Mungu. 12 Zile zilizo kando ya barabara ni wale ambao wamesikia, kisha Ibilisi huja na kuliondoa lile neno kutoka mioyoni mwao ili wasipate kuamini waokolewe. 13 Zile zilizo juu ya tungamo-mwamba ndio wale ambao, walisikiapo, hulipokea lile neno kwa shangwe, lakini hawa hawana mzizi; wao huamini kwa majira, lakini katika majira ya jaribu wao huanguka. 14 Kwa habari ya zile zilizoanguka katikati ya miiba, hawa ndio ambao wamesikia, lakini, kwa kuchukuliwa na mahangaiko na mali na raha za maisha haya, wao husongwa kabisa na hawakamilishi kitu. 15 Kwa habari ya zile zilizo penye udongo ulio bora, hawa ndio ambao, baada ya kusikia lile neno kwa moyo ulio bora na mwema, hulihifadhi na kuzaa matunda kwa uvumilivu.
16 “Hakuna yeyote, baada ya kuwasha taa, aifunikaye na chombo au kuiweka chini ya kitanda, bali huiweka juu ya kinara cha taa, ili wale wanaoingia ndani wapate kuiona nuru. 17 Kwa maana hakuna jambo lililofichwa ambalo halitakuwa dhahiri, wala kitu chochote kilichositiriwa kwa uangalifu ambacho hakitakuja kujulikana kamwe na ambacho hakitakuja kuwa wazi kamwe. 18 Kwa hiyo kazieni uangalifu jinsi msikilizavyo; kwa maana yeyote yule aliye na kitu, atapewa zaidi, lakini yeyote yule asiye na kitu, hata kile awaziacho kuwa anacho kitaondolewa mbali kutoka kwake.”
19 Sasa mama yake na ndugu zake wakaja kumwelekea, lakini hawakuweza kumfikia kwa sababu ya umati. 20 Hata hivyo, iliripotiwa kwake: “Mama yako na ndugu zako wamesimama nje wakitaka kukuona.” 21 Kwa kujibu akawaambia: “Mama yangu na ndugu zangu ni hawa wasikiao neno la Mungu na kulifanya.”
22 Baadaye katika mojawapo ya hizo siku yeye na wanafunzi wake waliingia katika mashua, naye akawaambia: “Na tuvuke hadi upande ule mwingine wa ziwa.” Kwa hiyo wakasafiri kwa mashua. 23 Lakini walipokuwa wakisafiri kwa mashua yeye akalala usingizi. Sasa dhoruba ya upepo wenye nguvu nyingi ikashuka juu ya ziwa, nao wakaanza kujawa na maji na kuwa katika hatari. 24 Mwishowe wakamwendea wakamwamsha, wakisema: “Mfunzi, Mfunzi, tuko karibu kuangamia!” Akijiamsha mwenyewe, akaukemea upepo na mchafuko wa maji, navyo vikatulia, kukawa shwari. 25 Ndipo akawaambia: “Imani yenu iko wapi?” Lakini wakiwa wameingiwa na hofu, wakastaajabu, wakiambiana: “Kwa kweli huyu ni nani, kwa maana aagiza hata pepo na maji, navyo humtii?”
26 Nao wakaegesha ufuoni katika nchi ya Wagerasene, iliyoko upande wa pili wa Galilaya. 27 Lakini alipotoka kwenye nchi kavu mwanamume fulani kutoka katika hilo jiji aliyekuwa na roho waovu akakutana naye. Na alikuwa hajavaa mavazi kwa muda mrefu, naye alikuwa akikaa, si nyumbani, bali katikati ya makaburi. 28 Alipomwona Yesu akalia kwa sauti kubwa akaanguka chini mbele yake, na kwa sauti kubwa akasema: “Mimi nina nini nawe, Yesu Mwana wa Mungu Aliye Juu Zaidi Sana? Nakuomba, usinitese-tese.” 29 (Kwa maana alikuwa amekuwa akiagiza huyo roho asiye safi amtoke huyo mtu. Kwa maana kwa muda mrefu alikuwa amemshika sana, naye alifungwa mara kwa mara kwa minyororo na pingu akiwa chini ya ulinzi, lakini akawa akivunja hivyo vifungo na kukimbizwa na huyo roho mwovu katika mahali pa upweke.) 30 Yesu akamuuliza: “Jina lako ni nani?” Akasema: “Lejioni,” kwa sababu roho wengi waovu walikuwa wamemwingia. 31 Nao wakafuliza kumsihi sana asiwaagize kwenda zao kuingia katika abiso. 32 Sasa idadi kubwa ya kundi la nguruwe ilikuwa ikilisha juu ya mlima; kwa hiyo wakamsihi sana awaruhusu waingie katika hao. Naye akawapa ruhusa. 33 Ndipo hao roho waovu wakaenda kutoka katika mtu huyo na kuingia katika wale nguruwe, na lile kundi likatimua mbio kali juu ya genge kuingia katika ziwa likafa maji. 34 Lakini wachungaji walipoona lililokuwa limetukia, wakakimbia na kuliripoti jijini na mashambani.
35 Ndipo watu wakatokea ili kuona lililokuwa limetukia, nao wakamjia Yesu wakamkuta yule mtu aliyetokwa na wale roho waovu, akiwa amevishwa na akiwa na akili yake timamu, ameketi miguuni pa Yesu; nao wakawa wenye hofu. 36 Wale waliokuwa wameona hilo wakaripoti kwao jinsi huyo mtu aliyepagawa na roho waovu alivyokuwa amefanywa apone. 37 Kwa hiyo umati wote kutoka nchi yenye kuzunguka ya Wagerasene ukamwomba aondoke kwao, kwa sababu ulikuwa umeshikwa na hofu kubwa. Ndipo akapanda ndani ya mashua na kurudi. 38 Hata hivyo, mwanamume ambaye roho waovu walikuwa wamemtoka akafuliza kumwomba ili aendelee kuwa pamoja naye; lakini yeye akamwagiza huyo mtu aende, akisema: 39 “Shika njia yako urudi nyumbani, na fuliza kusimulia mambo ambayo Mungu alikufanyia.” Basi akaenda zake, akipiga mbiu kotekote katika jiji lote mambo ambayo Yesu alimfanyia.
40 Yesu alipopata kurudi, umati ukampokea kwa fadhili, kwa maana wote walikuwa wakimtarajia. 41 Lakini, tazama! mwanamume aitwaye jina Yairo akaja, na mtu huyu alikuwa ofisa-msimamizi wa sinagogi. Naye akajiangusha miguuni pa Yesu akaanza kumsihi sana aingie katika nyumba yake, 42 kwa sababu alikuwa na binti mzaliwa-pekee mwenye umri wa miaka karibu kumi na miwili na alikuwa anakufa.
Alipokuwa akienda umati ukamsonga. 43 Na mwanamke, aliyeshikwa na mtiririko wa damu kwa miaka kumi na miwili, ambaye hakuwa ameweza kupata ponyo kutoka kwa yeyote, 44 akamkaribia kutoka nyuma akaugusa upindo wenye matamvua wa vazi lake la nje, na mara hiyo mtiririko wake wa damu ukakoma. 45 Kwa hiyo Yesu akasema: “Alikuwa nani aliyenigusa?” Wote walipokuwa wakikana hilo, Petro akasema: “Mfunzi, umati unakuzunguka na kukusonga sana.” 46 Lakini Yesu akasema: “Mtu fulani alinigusa, kwa maana nilihisi kwamba nguvu ilinitoka.” 47 Alipoona kwamba hakuponyoka kutambuliwa, huyo mwanamke akaja akitetemeka akaanguka chini mbele yake na kufunua mbele ya watu wote sababu ya yeye kumgusa na jinsi alivyoponywa mara hiyo. 48 Lakini yeye akamwambia: “Binti, imani yako imekufanya upone; shika njia yako uende katika amani.”
49 Alipokuwa bado akisema, mwakilishi fulani wa ofisa-msimamizi wa sinagogi akaja, akisema: “Binti yako amekufa; usimsumbue mwalimu tena.” 50 Aliposikia hilo, Yesu akamjibu: “Usiwe na hofu, weka imani tu, naye ataokolewa.” 51 Alipofika kwenye hiyo nyumba hakuacha yeyote aingie pamoja naye ila Petro na Yohana na Yakobo na baba na mama ya huyo msichana. 52 Lakini watu wote walikuwa wakitoa machozi na kujipiga-piga kwa kihoro kwa ajili yake. Kwa hiyo akasema: “Komeni kutoa machozi, kwa maana hakufa bali analala usingizi.” 53 Ndipo wakaanza kumcheka kwa kudharau, kwa sababu walijua alikuwa amekufa. 54 Lakini akamshika kwa mkono wake akaita, akisema: “Msichana, inuka!” 55 Na roho yake ikarudi, naye akainuka mara hiyo, na Yesu akaagiza apewe kitu ale. 56 Basi, wazazi wake wakapigwa na bumbuazi; lakini akawaagiza wasimwambie yeyote lililokuwa limetukia.