Ufunuo
17 Na mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na mabakuli saba akaja akanena nami, akisema: “Njoo, hakika mimi nitakuonyesha wewe hukumu juu ya kahaba mkubwa ambaye hukaa juu ya maji mengi, 2 ambaye wafalme wa dunia walifanya uasherati naye, lakini wale ambao huikaa dunia walifanywa walewe kwa divai ya uasherati wake.”
3 Naye akanichukua katika nguvu ya roho kuingia nyikani. Na nikaona mara hiyo mwanamke ameketi juu ya hayawani-mwitu wa rangi-nyekundu-nyangavu aliyejaa majina yenye makufuru na aliyekuwa na vichwa saba na pembe kumi. 4 Na huyo mwanamke alikuwa amepambwa nguo za rangi ya zambarau na nyekundu-nyangavu, na alikuwa amerembwa kwa dhahabu na jiwe lenye bei na lulu na mkononi mwake alikuwa na kikombe cha dhahabu kilichojaa mambo yenye kuchukiza sana na mambo yasiyo safi ya uasherati wake. 5 Na juu ya kipaji cha uso wake kulikuwa kumeandikwa jina, fumbo: “Babiloni Mkubwa, mama wa makahaba na wa mambo yenye kuchukiza sana ya dunia.” 6 Nami nikaona kwamba yule mwanamke amelewa damu ya watakatifu na damu ya mashahidi wa Yesu.
Basi, nilipomwona yeye mara hiyo nilistaajabu kwa staajabu kubwa. 7 Na kwa hiyo malaika akaniambia: “Kwa nini umestaajabu? Hakika nitakuambia fumbo la mwanamke na la hayawani-mwitu anayembeba na aliye na vichwa saba na pembe kumi: 8 Hayawani-mwitu uliyemwona alikuwako, lakini hayuko, na bado yuko karibu kupanda kutoka katika abiso, na ataondoka kwenda katika uharibifu. Na waonapo jinsi huyo hayawani-mwitu alivyokuwako, lakini hayuko, na hakika bado atakuwapo, wale ambao hukaa juu ya dunia watasifu kwa kumstaajabia, lakini majina yao hayajaandikwa juu ya hati-kunjo ya uhai tangu kuwekwa kwa msingi wa ulimwengu.
9 “Hapa ndipo akili iliyo na hekima yahitajiwa: Vichwa saba vyamaanisha milima saba, ambapo mwanamke huketi juu. 10 Na kuna wafalme saba: watano wameanguka, mmoja yuko, na mwingine bado hajawasili, lakini awasilipo lazima adumu kwa muda mfupi. 11 Na hayawani-mwitu aliyekuwako lakini hayuko, yeye mwenyewe pia ni mfalme wa nane, lakini huchipuka kutokana na wale saba, naye huondoka kwenda zake katika uharibifu.
12 “Na pembe kumi ulizoona zamaanisha wafalme kumi, ambao bado hawajapokea ufalme, lakini wapokea mamlaka wakiwa wafalme saa moja pamoja na hayawani-mwitu. 13 Hawa wana fikira moja, na kwa hiyo wampa hayawani-mwitu nguvu na mamlaka yao. 14 Hawa watapigana na Mwana-Kondoo, lakini, kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme, Mwana-Kondoo atawashinda. Pia, wale walioitwa na waliochaguliwa na walio waaminifu pamoja naye watafanya hivyo.”
15 Naye aniambia: “Maji uliyoyaona, aketipo kahaba, yamaanisha vikundi vya watu na umati na mataifa na lugha. 16 Nazo pembe kumi ulizoziona, na hayawani-mwitu, hawa watamchukia kahaba na watamfanya ukiwa na kuwa uchi, na watakula kabisa sehemu zake zenye nyama na watamchoma kabisa kwa moto. 17 Kwa maana Mungu alitia hilo ndani ya mioyo yao ili kutekeleza fikira yake, hata kutekeleza fikira yao moja kwa kumpa hayawani-mwitu ufalme wao, mpaka maneno ya Mungu yawe yamekwisha kutimizwa. 18 Na mwanamke uliyemwona amaanisha jiji kubwa lililo na ufalme juu ya wafalme wa dunia.”