Ufunuo
16 Nami nikasikia sauti kubwa kutoka katika patakatifu ikiwaambia hao malaika saba: “Nendeni mkamwage mabakuli saba ya hasira ya Mungu ndani ya dunia.”
2 Na wa kwanza akaenda zake akamwaga bakuli lake ndani ya dunia. Na kidonda chenye kuumiza na chenye kuleta dhara kikaja kuwa juu ya wanadamu waliokuwa na alama ya hayawani-mwitu na waliokuwa wakiabudu sanamu yake.
3 Na wa pili akamwaga bakuli lake ndani ya bahari. Nayo ikawa damu kama ya binadamu mfu, na kila nafsi iliyo hai ikafa, ndiyo, vitu vilivyomo baharini.
4 Na wa tatu akamwaga bakuli lake ndani ya mito na mabubujiko ya maji. Nayo ikawa damu. 5 Nami nikasikia malaika aliye juu ya yale maji akisema: “Wewe, Uliyeko na uliyekuwako, Mwaminifu-Mshikamanifu, ni mwadilifu, kwa sababu umetoa maamuzi haya, 6 kwa sababu walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wanywe. Wao wastahili hilo.” 7 Nami nikasikia madhabahu ikisema: “Ndiyo, Yehova Mungu, Mweza-Yote, ni ya kweli na ya uadilifu maamuzi yako ya kihukumu.”
8 Na wa nne akamwaga bakuli lake juu ya jua; na jua likapewa ruhusa ya kuunguza wanadamu kwa moto. 9 Nao wanadamu wakaunguzwa kwa joto kubwa, lakini wakakufuru jina la Mungu, aliye na mamlaka juu ya tauni hizi, nao hawakutubu ili wampe utukufu.
10 Na wa tano akamwaga bakuli lake juu ya hicho kiti cha ufalme cha hayawani-mwitu. Na ufalme wake ukawa wenye kutiwa giza, nao wakaanza kuguguna ndimi zao kwa umivu lao, 11 lakini wakakufuru Mungu wa mbinguni kwa maumivu yao na kwa vidonda vyao, nao hawakutubu juu ya kazi zao.
12 Na wa sita akamwaga bakuli lake juu ya mto mkubwa Eufrati, na maji yao yakakauka kabisa, ili njia ipate kutayarishwa kwa ajili ya wafalme watokao macheo ya jua.
13 Nami nikaona semi zisizo safi tatu zilizopuliziwa ambazo zilionekana kama vyura zikitoka katika kinywa cha joka kubwa na kutoka kinywani mwa hayawani-mwitu na kutoka kinywani mwa nabii asiye wa kweli. 14 Kwa kweli, hizo ndizo semi zilizopuliziwa na roho waovu na zafanya ishara, nazo zatoka kwenda kwa wafalme wa dunia nzima inayokaliwa, kuwakusanya pamoja kwa vita ya siku kubwa ya Mungu Mweza-Yote.
15 “Tazama! Ninakuja kama mwizi. Mwenye furaha ni yeye akaaye macho na hutunza mavazi yake ya nje, ili asipate kutembea akiwa uchi na watu waitazame hali yake ya aibu.”
16 Nazo zikawakusanya pamoja mahali paitwapo katika Kiebrania Har-Magedoni.
17 Na wa saba akamwaga bakuli lake juu ya hewa. Ndipo sauti kubwa ikatokea patakatifu kutoka kiti cha ufalme, ikisema: “Imekuwa!” 18 Na meme na sauti na ngurumo zikatokea, na tetemeko kubwa la dunia likatukia la namna ambayo haijatukia tangu wanadamu walipokuja kuwa duniani, tetemeko la dunia lenye kuenea sana, lililo kubwa sana. 19 Na jiji kubwa likapasuka kuwa sehemu tatu, na majiji ya mataifa yakaanguka; na Babiloni Mkubwa akakumbukwa machoni pa Mungu, kumpa kikombe cha divai cha hasira ya hasira yake ya kisasi. 20 Pia, kila kisiwa kikakimbia, na milima haikupatikana. 21 Na mvua kubwa ya mawe yenye kila jiwe likiwa na uzani wa karibu talanta moja ikashuka kutoka mbinguni juu ya wanadamu, na hao wanadamu wakakufuru Mungu kwa sababu ya tauni ya hiyo mvua ya mawe, kwa sababu tauni yayo ilikuwa kubwa isivyo kawaida.