Ufunuo
13 Nalo likasimama tuli juu ya mchanga wa bahari.
Nami nikaona hayawani-mwitu akipanda kutoka katika bahari, mwenye pembe kumi na vichwa saba, na juu ya pembe zake vilemba kumi, lakini juu ya vichwa vyake majina yenye kufuru. 2 Sasa yule hayawani-mwitu niliyemwona alikuwa kama chui, lakini miguu yake ilikuwa kama ile ya dubu, na kinywa chake kilikuwa kama kinywa cha simba. Na joka kubwa likampa huyo hayawani nguvu yake na hicho kiti chake cha ufalme na mamlaka kubwa.
3 Nami nikaona kimoja cha vichwa vyake kama kwamba kilichinjwa hadi kifo, lakini pigo lacho la kifo likapona, na dunia yote ikamfuata hayawani-mwitu kwa kumstaajabia. 4 Nao wakaliabudu joka kubwa kwa sababu lilimpa hayawani-mwitu mamlaka, nao wakamwabudu hayawani-mwitu kwa maneno haya: “Ni nani aliye kama hayawani-mwitu, na ni nani awezaye kupigana naye?” 5 Naye akapewa kinywa chenye kusema mambo makubwa na makufuru, naye akapewa mamlaka ya kutenda miezi arobaini na miwili. 6 Naye akafungua kinywa chake kwa makufuru dhidi ya Mungu, kukufuru jina lake na makao yake, hata wale wanaokaa mbinguni. 7 Naye akapewa ruhusa ya kufanya vita na watakatifu na kuwashinda, naye akapewa mamlaka juu ya kila kabila na watu na lugha na taifa. 8 Na wote wale wakaao juu ya dunia watamwabudu; hakuna jina la hata mmoja wao ambalo limeandikwa katika hati-kunjo ya uhai ya Mwana-Kondoo aliyechinjwa, tangu kuwekwa kwa msingi wa ulimwengu.
9 Ikiwa yeyote ana sikio, acheni asikie. 10 Ikiwa yeyote amekusudiwa utekwa, yeye huenda zake katika utekwa. Ikiwa yeyote ataua kwa upanga, yeye lazima atauawa kwa upanga. Hapa ndipo humaanisha uvumilivu na imani ya watakatifu.
11 Nami nikaona hayawani-mwitu mwingine akipanda kutoka katika dunia, naye alikuwa na pembe mbili kama mwana-kondoo, lakini akaanza kusema kama joka kubwa. 12 Naye hutumia mamlaka yote ya hayawani-mwitu wa kwanza mbele ya macho yake. Naye hufanya dunia na wale ambao hukaa ndani yayo kuabudu huyo hayawani-mwitu wa kwanza, ambaye pigo lake la kifo lilipona. 13 Naye hufanya ishara zilizo kubwa, hivi kwamba afanye hata moto uteremke kutoka mbinguni hadi kwenye dunia machoni pa wanadamu.
14 Naye huongoza vibaya wale wakaao juu ya dunia, kwa sababu ya ishara alizopewa ruhusa kufanya mbele ya macho ya hayawani-mwitu, huku akiwaambia wale wakaao juu ya dunia wafanye sanamu ya hayawani-mwitu aliyekuwa na pigo la upanga na bado akarudia uhai. 15 Naye akaruhusiwa kuipa pumzi sanamu ya hayawani-mwitu, ili hiyo sanamu ya hayawani-mwitu iseme na pia kusababisha wauawe wale wote ambao katika njia yoyote hawakutaka kuiabudu sanamu ya hayawani-mwitu.
16 Naye huwashurutisha watu wote, walio wadogo na wakubwa, na matajiri na maskini, na walio huru na watumwa, ili wawape alama katika mkono wao wa kuume au juu ya kipaji cha uso wao, 17 na ili mtu yeyote asiweze kununua au kuuza ila mtu aliye na alama, jina la hayawani-mwitu au nambari ya jina lake. 18 Hapa ndipo hekima yahitajiwa: Acheni aliye na akili apige hesabu ya nambari ya huyo hayawani-mwitu, kwa maana ni nambari ya binadamu; na nambari yake ni mia sita sitini na sita.