Mathayo
17 Siku sita baadaye Yesu alichukua pamoja naye Petro na Yakobo na Yohana ndugu yake akawaleta juu katika mlima ulioinuka sana wakiwa peke yao wenyewe. 2 Naye akageuka umbo mbele yao, na uso wake ukang’aa kama jua, na mavazi yake ya nje yakawa maangavu kama nuru. 3 Na, tazama! kukaonekana kwao Musa na Eliya, wakiongea naye. 4 Kwa kujibu Petro akamwambia Yesu: “Bwana, ni vizuri kwetu kuwa hapa. Ukitaka, hakika nitasimamisha mahema matatu hapa, moja lako na moja la Musa na moja la Eliya.” 5 Alipokuwa bado akisema, tazama! wingu jangavu liliwafunika kivuli, na, tazama! sauti kutoka katika lile wingu, ikisema: “Huyu ni Mwana wangu, mpendwa, ambaye mimi nimemkubali; msikilizeni yeye.” 6 Waliposikia hilo wanafunzi wakaanguka kifudifudi na kuwa wenye kuogopa sana. 7 Ndipo Yesu akaja karibu na, akiwagusa, akasema: “Inukeni na msiwe na hofu.” 8 Walipoinua macho yao, hawakuona yeyote ila Yesu mwenyewe tu. 9 Na walipokuwa wakishuka kutoka kwenye huo mlima, Yesu akawaamuru, akisema: “Msiambie yeyote hilo ono mpaka Mwana wa binadamu afufuliwe kutoka kwa wafu.”
10 Hata hivyo, wanafunzi wakamtokezea swali hili: “Basi, kwa nini waandishi husema kwamba ni lazima Eliya aje kwanza?” 11 Kwa kujibu yeye akasema: “Eliya, kwa kweli, anakuja naye atarudisha mambo yote. 12 Hata hivyo, mimi nawaambia nyinyi kwamba tayari Eliya amekuja nao hawakumtambua bali walimfanya mambo waliyotaka. Katika njia hiyo pia Mwana wa binadamu akusudiwa kuteseka mikononi mwao.” 13 Ndipo wanafunzi wakafahamu kwamba aliwaambia juu ya Yohana Mbatizaji.
14 Nao walipokuja kuuelekea umati, mtu fulani akamkaribia, akimpigia magoti na kusema: 15 “Bwana, uwe na rehema juu ya mwana wangu, kwa sababu yeye ni mwenye kifafa na ni mgonjwa, kwa maana yeye huanguka mara nyingi ndani ya moto na mara nyingi ndani ya maji; 16 nami nilimleta kwa wanafunzi wako, lakini hawakuweza kumponya.” 17 Kwa kujibu Yesu akasema: “Ewe kizazi kisicho na imani na kilichopotoka, ni kwa muda gani lazima niendelee kuwa pamoja nanyi? Ni kwa muda gani lazima nichukuliane nanyi? Mleteni hapa kwangu.” 18 Ndipo Yesu akamkemea, na huyo roho mwovu akatoka ndani yake; na huyo mvulana akaponywa tangu saa hiyo. 19 Hapo wanafunzi wakamjia Yesu kwa faragha na kusema: “Ni kwa nini sisi hatukuweza kumfukuza?” 20 Yeye akawaambia: “Kwa sababu ya imani yenu kidogo, kwa maana kwa kweli nawaambia nyinyi, Mkiwa na imani yenye ukubwa wa punje ya haradali, mtaambia mlima huu, ‘Hama kutoka hapa hadi pale,’ nao utahama, na hakuna jambo litakalokuwa haliwezekani kwenu.” 21 ——
22 Ilikuwa ni wakati walipokuwa wamekusanyika pamoja katika Galilaya kwamba Yesu akawaambia: “Mwana wa binadamu amekusudiwa kusalitiwa mikononi mwa watu, 23 nao watamuua, na siku ya tatu atafufuliwa.” Kwa sababu hiyo wakatiwa kihoro sana.
24 Baada ya wao kuwasili katika Kapernaumu watu wenye kukusanya [kodi] ya drakma mbili wakamkaribia Petro na kusema: “Je, mwalimu wenu halipi [kodi] ya drakma mbili?” 25 Akasema: “Ndiyo.” Hata hivyo, alipoingia ndani ya nyumba Yesu alimtangulia kwa kusema: “Wewe wafikiri nini, Simoni? Ni kutoka kwa nani wafalme wa dunia hupokea ushuru wa forodhani au kodi ya kichwa? Ni kutoka kwa wana wao au ni kutoka kwa wageni?” 26 Aliposema: “Kutoka kwa wageni,” Yesu akamwambia: “Basi, kwa kweli hao wana hawalipi kodi. 27 Lakini ili tusisababishe wakwazike, wewe nenda kwenye bahari, tupa ndoana, nawe chukua samaki wa kwanza anayetokea na, ufunguapo kinywa chake, utapata sarafu ya stateri. Ichukue na uwape hiyo kwa ajili yangu na wewe.”