Mathayo
18 Katika saa hiyo wanafunzi wakaja karibu na Yesu na kusema: “Ni nani kwa kweli aliye mkubwa zaidi sana katika ufalme wa mbingu?” 2 Basi, akiita mtoto mchanga kwake, akamweka katikati yao 3 na kusema: “Kwa kweli nawaambia nyinyi, Msipogeuka kabisa na kuwa kama watoto wachanga, hamtaingia kwa vyovyote katika ufalme wa mbingu. 4 Basi, yeyote atakayejinyenyekeza mwenyewe kama mtoto mchanga huyu ndiye aliye mkubwa zaidi sana katika ufalme wa mbingu; 5 na yeyote yule apokeaye mtoto mchanga mmoja wa namna hii juu ya msingi wa jina langu anipokea mimi pia. 6 Lakini yeyote yule akwazaye mmoja wa wadogo hawa wawekao imani katika mimi, ni jambo lenye manufaa zaidi kwake jiwe la kusagia kama lile lizungushwalo na punda lining’inizwe kuzunguka shingo yake na kuzamishwa katika bahari pana, iliyo wazi.
7 “Ole wao ulimwengu kwa sababu ya vipingamizi vyenye kukwaza! Bila shaka, hivyo vipingamizi vyenye kukwaza ni lazima vije, lakini ole wake mtu ambaye kupitia yeye kipingamizi chenye kukwaza huja! 8 Basi, ikiwa mkono wako au mguu wako unakufanya ukwazike, ukatilie mbali na kuutupilia mbali nawe; ni vizuri zaidi kwako kuingia katika uhai ukiwa umeharibika viungo au ukiwa kilema kuliko kutupwa ndani ya moto udumuo milele ukiwa na mikono miwili au miguu miwili. 9 Pia, ikiwa jicho lako linakufanya ukwazike, ling’oe kabisa na ulitupilie mbali nawe; ni vizuri zaidi kwako kuingia katika uhai ukiwa na jicho moja kuliko kutupwa ndani ya Gehena ya moto ukiwa na macho mawili. 10 Angalieni kwamba nyinyi watu hamdharau mmoja wa wadogo hawa; kwa maana nawaambia nyinyi kwamba malaika zao mbinguni sikuzote huuona uso wa Baba yangu aliye mbinguni. 11 ——
12 “Nyinyi mwafikiri nini? Ikiwa mtu fulani aja kuwa na kondoo mia moja na mmoja wao apotea njia, je, hataacha wale tisini na tisa juu ya milima na kuondoka kwenda kutafuta yule anayepotea njia? 13 Na ikitukia ampate, mimi nawaambia nyinyi hakika, yeye hushangilia zaidi juu ya huyo kuliko juu ya wale tisini na tisa ambao hawajapotea njia. 14 Hivyohivyo si jambo la kutamanika kwa Baba yangu aliye mbinguni kwa mmoja wa wadogo hawa kuangamia.
15 “Zaidi ya hayo, ndugu yako akifanya dhambi, nenda ufunue wazi kosa lake kati yako na yeye peke yake. Akikusikiliza, umempata ndugu yako. 16 Lakini ikiwa yeye hasikilizi, chukua pamoja nawe mmoja au wawili zaidi, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila jambo lipate kuthibitishwa. 17 Ikiwa yeye hawasikilizi wao, liambie kutaniko. Ikiwa hasikilizi hata kutaniko, mwache awe kwako kama vile mtu wa mataifa na kama mkusanya-kodi.
18 “Kwa kweli nawaambia nyinyi watu, Mambo yoyote yale ambayo huenda mkafunga duniani yatakuwa mambo yaliyofungwa mbinguni, na mambo yoyote yale ambayo huenda mkafungua duniani yatakuwa mambo yaliyofunguliwa mbinguni. 19 Tena nawaambia nyinyi kweli, Ikiwa wawili kati yenu duniani wapatana kuhusu jambo lolote lenye maana wapaswalo kuomba, litatendeka kwao kwa sababu ya Baba yangu aliye mbinguni. 20 Kwa maana palipo na wawili au watatu wakiwa wamekusanyika pamoja katika jina langu, hapo mimi nipo katikati yao.”
21 Ndipo Petro akaja na kumwambia: “Bwana, ni mara ngapi ndugu yangu atafanya dhambi dhidi yangu nami nimsamehe? Mpaka mara saba?” 22 Yesu akamwambia: “Nakuambia, si, Mpaka mara saba, bali, Mpaka mara sabini na saba.
23 “Hiyo ndiyo sababu ufalme wa mbingu umekuwa kama mtu, mfalme, aliyetaka kufanya hesabu pamoja na watumwa wake. 24 Alipoanza kuzifanya, kuliletwa ndani mtu ambaye aliwiwa naye talanta elfu kumi [=dinari 60,000,000]. 25 Lakini kwa sababu hakuwa na uwezo wa kuilipa, bwana-mkubwa wake akaagiza yeye na mke wake na watoto wake na vitu vyote alivyokuwa navyo wauzwe na malipo yafanywe. 26 Kwa hiyo huyo mtumwa akaanguka chini na kuanza kumsujudia, akisema, ‘Uwe mwenye subira kwangu nami hakika nitakulipa kila kitu.’ 27 Akisikitishwa na hayo, bwana-mkubwa wa mtumwa huyo akamwachilia na kufuta deni lake. 28 Lakini mtumwa huyo akatoka kwenda na kukuta mmoja wa watumwa wenzake aliyekuwa anamwia dinari mia; na, akimbamba, akaanza kumsonga pumzi, akisema, ‘Lipa chochote kile uwiwacho.’ 29 Kwa hiyo mtumwa mwenzake akaanguka chini na kuanza kumsihi sana, akisema, ‘Uwe mwenye subira kwangu nami hakika nitakulipa.’ 30 Hata hivyo, yeye hakutaka, bali akaenda zake na kufanya atupwe gerezani mpaka alipe kilichokuwa kinawiwa. 31 Kwa hiyo, watumwa wenzake walipoona mambo yaliyokuwa yametukia, walitiwa kihoro sana, nao wakaenda na kuelewesha wazi kwa bwana-mkubwa wao mambo yote yaliyokuwa yametukia. 32 Ndipo bwana-mkubwa wake akamwita na kumwambia, ‘Mtumwa mwovu, nilifuta deni lote lile kwa ajili yako, uliponisihi sana. 33 Haikukupasa wewe, nawe, kuwa na rehema juu ya mtumwa mwenzako, kama mimi pia nilivyokuwa na rehema juu yako?’ 34 Ndipo bwana-mkubwa wake, kwa kuchokozwa kuwa na hasira ya kisasi, akamkabidhi kwa walinzi wa jela, mpaka alipe vyote vilivyokuwa vikiwiwa. 35 Kwa njia kama hiyo Baba yangu wa kimbingu atashughulika nanyi pia ikiwa hamsamehi kila mmoja ndugu yake kutoka katika mioyo yenu.”