Ufunuo
21 Nami nikaona mbingu mpya na dunia mpya; kwa maana mbingu ya kwanza na dunia ya kwanza zilikuwa zimepitilia mbali, na bahari haipo tena. 2 Nikaona pia jiji takatifu, Yerusalemu Jipya, likiteremka kutoka mbinguni kwa Mungu na limetayarishwa kama bibi-arusi aliyerembwa kwa ajili ya mume wake. 3 Ndipo nikasikia sauti kubwa kutoka katika kiti cha ufalme ikisema: “Tazama! Hema la Mungu liko pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao, nao watakuwa vikundi vya watu wake. Na Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. 4 Naye atafuta kabisa kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala ombolezo wala kupaaza kilio wala umivu halitakuwapo tena kamwe. Mambo ya zamani yamepitilia mbali.”
5 Na Yeye aketiye juu ya kiti cha ufalme akasema: “Tazama! Mimi ninafanya vitu vyote kuwa vipya.” Pia, husema: “Andika, kwa sababu maneno haya ni ya uaminifu na ya kweli.” 6 Naye akasema nami akaniambia: “Yamekuwa! Mimi ndiye Alfa na Omega, mwanzo na mwisho. Kwa yeyote aliye na kiu hakika mimi nitampa kutoka kwenye bubujiko la maji ya uhai bure. 7 Yeyote anayeshinda atarithi vitu hivi, nami nitakuwa Mungu wake naye atakuwa mwana wangu. 8 Lakini kwa habari ya waoga na wale wasio na imani na wale wenye kuchukiza sana katika uchafu wao na wauaji-kimakusudi na waasherati na wale wanaozoea kuwasiliana na roho na waabudu-sanamu na waongo wote, fungu lao litakuwa ndani ya ziwa liwakalo moto na sulfa. Hili humaanisha kifo cha pili.”
9 Na akaja mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na mabakuli saba yaliyojaa tauni saba za mwisho, naye akasema nami na kuniambia: “Njoo hapa, hakika nitakuonyesha bibi-arusi, mke wa Mwana-Kondoo.” 10 Kwa hiyo akanichukua mbali katika nguvu ya roho hadi kwenye mlima mkubwa na ulioinuka juu sana, naye akanionyesha jiji takatifu Yerusalemu likiteremka kutoka mbinguni kutoka kwa Mungu 11 na likiwa na utukufu wa Mungu. Mnururisho walo ulikuwa kama jiwe lenye bei zaidi sana, kama jiwe la yaspi lenye kung’aa kwa uangavu kama fuwele. 12 Lilikuwa na ukuta mkubwa na ulioinuka juu sana na lilikuwa na malango kumi na mawili, na kwenye hayo malango malaika kumi na wawili, na majina yalikuwa yameandikwa ambayo ni yale ya makabila kumi na mawili ya wana wa Israeli. 13 Upande wa mashariki kulikuwa na malango matatu, na upande wa kaskazini malango matatu, na upande wa kusini malango matatu, na upande wa magharibi malango matatu. 14 Ukuta wa jiji pia ulikuwa na mawe ya msingi kumi na mawili, na juu yayo majina kumi na mawili ya mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo.
15 Sasa yeye aliyekuwa akisema nami alikuwa ameshika tete la dhahabu kuwa kipimio, ili apate kupima jiji na malango yalo na ukuta walo. 16 Na jiji lakaa miraba minne, na urefu walo ni mkubwa sawasawa na upana walo. Naye akapima jiji kwa tete, stadia elfu kumi na mbili; urefu na upana walo na kimo chalo ni sawa. 17 Pia, akapima ukuta walo, dhiraa mia na arobaini na nne, kulingana na kipimo cha mwanadamu, wakati huohuo cha malaika. 18 Basi muundo wa ukuta walo ulikuwa yaspi, na jiji lilikuwa dhahabu yenye kutakata kama kioo safi. 19 Misingi ya ukuta wa jiji ilikuwa imerembwa kwa kila namna ya jiwe lenye bei: msingi wa kwanza ulikuwa yaspi, wa pili yakuti, wa tatu kalkedoni, wa nne zumaridi, 20 wa tano sardoniksi, wa sita sardio, wa saba krisolito, wa nane beroli, wa tisa topazi, wa kumi krisopraso, wa kumi na moja hayasinthi, wa kumi na mbili amethisto. 21 Pia, malango kumi na mawili yalikuwa lulu kumi na mbili; kila moja la malango lilikuwa limefanywa kwa lulu moja. Na njia pana ya jiji ilikuwa dhahabu yenye kutakata, kama kioo chenye kuona.
22 Nami sikuona hekalu katika hilo, kwa maana Yehova Mungu Mweza-Yote ndiye hekalu lalo, pia Mwana-Kondoo. 23 Na jiji halina uhitaji wowote wa jua wala wa mwezi kung’aa juu yalo, kwa maana utukufu wa Mungu ulilinurisha, na taa yalo ilikuwa ni Mwana-Kondoo. 24 Na mataifa yatatembea kwa njia ya nuru yalo, na wafalme wa dunia wataleta utukufu wao ndani yalo. 25 Na malango yalo hayatafungwa hata kidogo wakati wa mchana, kwa maana usiku hautakuwako huko. 26 Nao wataleta utukufu na heshima ya mataifa ndani yalo. 27 Lakini kitu chochote kisicho kitakatifu na yeyote ambaye huendeleza kitu chenye kuchukiza sana na uwongo hataingia kwa njia yoyote ndani yalo; ila tu wale ambao wameandikwa katika hati-kunjo ya uhai ya Mwana-Kondoo.